Madrid, Hispania
Rais wa klabu ya Barcelona, Joan Laporta alilazimika kuombwa aondoke kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kutaka waamuzi wampe maelezo kuhusu baadhi ya maamuzi katika mechi yao na Real Madrid maarufu El Clasico.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumapili kwenye dimba la Santiago Bernabeu, Barca ililala kwa mabao 3-1, matokeo yanayoifanya Real Madrid kushika usukani wa La Liga na kuiacha Barca katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tatu.
Awali katika mechi hiyo Barca ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kabla ya kuibua matumaini kwa bao la Ferran Torres na matokeo kusomeka 2-1 lakini penalti ya dakika ya 83 iliyotolewa baada ya Eric Garcia kumchezea rafu Rodrygo iliiwezesha Real Madrid kupata bao la tatu mfungaji akiwa Rodrygo. Mabao mengine ya Real Madrid yalifungwa na Karim Benzema na Federico Valverde.
Penalti hiyo iliibua hasira kwa mashabiki wa Barca wakiamini haikuwa halali ingawa mwamuzi huyo alijiridhisha kwa kuangalia picha kabla ya kuipa Real Madrid penalti lakini kilichowakera zaidi Barca ni wao kunyimwa penalti hapo kabla baada ya Robert Lewandowski kuchezewa rafu na Dani Carvajal na mwamuzi hakutaka japo kujiridhisha kwa kuangalia picha ili kuwa na uhakika.
“Baada ya mechi kumalizika na timu ya waamuzi ikiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Rais wa Barca, Laporta alikuja na kuuliza mara mbili mbili akitaka ufafanuzi kuhusu muda wa nyongeza katika mechi. Laporta alitakiwa kuondoka katika eneo hilo bila ya kutokea matukio yoyote mengine,” ripoti ya waamuzi wa mechi hiyo ilieleza.
Hatua ya Laporta imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kocha wa Barca, Xavi Hernandez kunukuliwa akisema kwamba waamuzi wanatakiwa kufanya mikutano na waandishi wa habari baada ya mechi kwa kile alichodai ni kutotendewa haki kwa timu yake katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan, mechi ambayo Barca walipoteza.
Xavi hata hivyo hakusema lolote kuhusu waamuzi baada ya timu yake kupoteza mechi dhidi ya Real Madrid badala yake alizungumzia juhudi ilizofanya timu hiyo na kwamba kilichotokea ni timu kutokuwa na bahati.
Kimataifa Rais Barca awavaa waamuzi El Clasico
Rais Barca awavaa waamuzi El Clasico
Related posts
Read also