Na mwandishi wetu
Simba hii ya kimataifa, ndivyo unavyoweza kusema, ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola unatoa ishara ya dhamira ya Simba kufika mbali kimataifa msimu huu.
Ushindi wa Simba ambao umepatikana Jumapili hii umekuja baada ya timu hiyo kuanza kwa mafanikio hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitoa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0, ikiwa ni mafanikio ya awali ya Simba kimataifa na kwa ushindi wa De Agosto si vibaya kuitabiria Simba kufikia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo au zaidi ya hapo.
Alikuwa ni Mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama ambaye aliiandikia Simba bao la kwanza katika dakika ya 10 na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao hilo kabla Israel Mwenda hajaandika bao la pili katika dakika ya 62.
Mosses Phiri aliongeza bao la tatu kwa Simba katika dakika ya 76 kabla De Agosto hawajapata bao pekee la kufutia machozi dakika tatu baadaye.
Ushindi wa leo si tu kwamba unazidi kuipa Simba heshima lakini pia unazidi kuinua hadhi ya kocha Juma Mgunda ambaye ameichukua timu hiyo akiwa kocha wa muda lakini kwa kazi ambayo ameifanya hadi sasa hapana shaka anastahili heshima na kuaminiwa na mabosi wa klabu ya Simba kwa kupewa mkataba wa kudumu.
Kimataifa Simba hii ya kimataifa
Simba hii ya kimataifa
Related posts
Read also