Madrid, Hispania
Mabosi La Liga wameingilia kati sakata la mchezaji wa Real Madrid, Vinicius Jr kutolewa kauli za kibaguzi na mashabiki na kuahidi kushirikiana na mamlaka kuwakamata wahusika.
Tukio hilo lilitokea Jumapili katika mechi ya Real Madrid dhidi ya mahasimu wao Atletico Madrid na Real kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambapo baadhi ya mashabiki inadaiwa waliimba nyimbo za kumsakama mchezaji huyo zilizokuwa na maudhui ya kibaguzi.
“Tunalaani matukio yote ya ndani na nje ya viwanja, tunafanya kazi na klabu ili kulifanya soka letu liwe la kirafiki na burudani, kauli zote za chuki hazina nafasi katika La Liga na wakati wote tunafanya kazi na klabu na mamlaka ili kuwabaini wahusika na kuhakikisha haki inatendeka katika matukio hayo,” ilieleza taarifa ya La Liga.
Katika siku za karibuni, Vinicius amekuwa na tabia ya kushangilia bao anapofunga kwa staili ya kucheza, staili ambayo imeibua maoni mbalimbali kutoka kwa wachambuzi wa soka wa Hispania.
Wakala, Pedro Bravo alisema kwamba nchini Hispania unatakiwa kuheshimu timu pinzani na kuacha kufanya michezo ya nyani na huo kuwa mwanzo wa kuibua tuhuma za kauli za kibaguzi ingawa Pedro aliomba msamaha.
Vinicius ambaye ni Mbrazili tayari amefunga mabao matano katika mechi nane msimu huu, katika taarifa yake aliyoitoa Ijumaa aliwataja mastaa wengine wa soka ambao wamekuwa wakiitumia staili hiyo ya kucheza hasa wanapofunga.
“Wiki chache zilizopita baadhi ya watu wamekuwa wakikosoa aina muziki ninaocheza, lakini huo si aina ya uchezaji wangu peke yangu, ni wa Ronaldinho, Neymar, Paqueta, Griezmann, Joao Felix, Matheus Cunha na Wabrazil wengine, wanamuziki na madansa wa samba, ni dansi la kufurahia tamasha la muingiliano wa kiutamaduni duniani,” alisema Vinicius.
“Wanasema furaha ya aina hiyo inawakera, furaha ya Mbrazili mweusi anayepata mafanikio Ulaya inawakera zaidi lakini dhamira yangu ya kutaka ushindi, tabasamu langu ni mambo makubwa kuliko hilo,” aliongeza mchezaji huyo.
Vinicius aliungwa mkono na wachezaji kadhaa wa Brazil kwenye mitandao ya kijamii wakiwamo Pele na Neymar wakati klabu ya Real Madrid imetoa taarifa ikishutumu kauli za wachambuzi wa soka zilizotolewa Ijumaa.
Shutuma zote na matukio ya kibaguzi havikumzuia Vinicius na Mbrazil mwenzake wa Real Madrid, Rodrygo kucheza kwa staili hiyo hiyo ilyoibua kero baada ya Rodrygo kufunga goli.
Kimataifa La Liga watoa neno sakata la Vinicius Jr
La Liga watoa neno sakata la Vinicius Jr
Related posts
Read also