New York, Marekani
Staa wa tenisi, Serena Williams amempongeza staa mwenzake, Roger Federer kwa uamuzi wa kustaafu akimkaribisha katika klabu ya wastaafu na kumsifia kwa kuchangia kutoa hamasa katika mchezo huo.
“Umewahamasisha mamilioni ya watu nikiwamo mimi na hilo hatutaweza kulisahau, karibu katika klabu ya wastaafu, na ahsante kwa kuendelea kuwa wewe yule yule,” alisema Serena ambaye naye tayari ametangaza dhamira ya kustaafu akiwa ameshinda karibu kila kitu katika mchezo huo kama ilivyo kwa Federer.
Federer ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 41 atastaafu rasmi mchezo wa tenisi baada ya mashindano ya Laver Cup ambayo yatafanyika katika jiji la London kuanzia Septemba 23 mwaka huu.
“Wakati wote nimekuwa nikikuangalia wewe na kuvutiwa na wewe, nakupongeza na nasubiri ili kushuhudia yote ambayo umepanga kuyafanya katika siku zijazo,” alisema Serena.
Uamuzi wa Federer kustaafu tenisi pamoja na mambo mengine umechangiwa na majeraha ya goti ambayo yamekuwa yakimuandama kwa takriban miaka mitatu sasa.
Mpinzani wa Federer, Rafael Nadal ambaye kama alivyo Federer ni kati ya wacheza tenisi wenye Grand Slam nyingi, aliutaja uamuzi wa Federer kuwa ni siku ya huzuni katika mchezo huo.
Mabingwa namba moja wa dunia katika tenisi Iga Swiatek (21) na Carlos Alcaraz (19) wote kwa pamoja walimshukuru Federer kwa namna alivyowahamasisha katika mchezo wa tenisi.
“Ninataka kukushukuru kwa kila kitu ulichofanya, na kwa kila namna ambavyo umekuwa katika mchezo wetu huu, ni bahati ya kipekee kukushuhudia wewe katika tenisi,” alisema Swiatek.
Naye Alcaraz alisema: “Roger amekuwa shujaa wangu na chanzo cha hamasa, ahsante kwa kila kitu ulichofanya katika mchezo wetu, bado nataka kucheza na wewe.”
Sports Mix Serena amkaribisha Federer katika klabu ya wastaafu
Serena amkaribisha Federer katika klabu ya wastaafu
Read also
