Na mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pamela Gekul ameeleza kuwa wapo kwenye mchakato wa kutazama gharama ili kuirejesha Ligi ya Muungano kwa ajili ya kuboresha afya ya timu ya taifa na ushindani kwa taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo na Gekul alipokuwa bungeni wakati akijibu swali la Mbunge Suleiman Haroub Suleiman aliyehitaji kujua lini Ligi ya Muungano itarejea ambayo uhusisha timu za Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Naibu Waziri alieleza kuwa kabla ya kuulizwa swali hilo tayari wizara ilishaona umuhimu wa kurejea kwa ligi hiyo ambayo ilifanyika mara ya mwisho takriban miaka 19 iliyopita, hivyo tayari wapo kwenye mazungumzo na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ili kuhakikisha wanairejesha ligi hiyo.
“Kwa niaba ya Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo (Mohamed Mchengerwa) jambo hili kama wizara tumeliona, tumekua na mazungumzo baina ya BMT, TFF na ZFF kuhakikisha ligi hii inarudishwa…
“Mwanzoni ilisitishwa kwa sababu Zanzibar ilipata ushirika wa uanachama wa Caf (Shirikisho la Soka Afrika) wakawa wanapeleka timu zao mbili na Bara ikawa inapeleka mbili, lakini kwa afya ya muungano wetu na ushirikiano tulionao kama taifa tumekubaliana na kamati ishaundwa ligi hii itarudishwa hivi karibuni, tunaangalia tu tathmini ya gharama kwamba gharama zitakuwaje lakini itarudishwa,” alisema Gekul.
Pia, Waziri Gekul alieleza namna Zanzibar inavyoshirikishwa katika uundwaji wa timu ya taifa na kwamba hakuna mipaka ya kocha wa Taifa Stars kuangalia ni ligi ipi aite mchezaji kama ambavyo Mbunge Suleiman alivyotaka ufafanuzi kuhusu uteuzi pia wa kikosi cha Stars kwa wachezaji wa Ligi ya Zanzibar.
“Tunapochagua wachezaji wa timu ya taifa, kocha hakatazwi kwenda kokote kwenye hizi ligi ndani ya taifa letu na hili limekuwa likifanyika ndiyo maana wachezaji katika timu yetu ya taifa wanatoka pia Zanzibar na pia Bara.
“Kwa hiyo hili tutaendelea kuliimarisha tukishirikiana na ZFF pamoja na TFF kuhakikisha tunapata wachezaji wazuri na hata katika benchi la ufundi tumekuwa tukihusisha wenzetu wa Zanzibar kuhakikisha wanatoa mchango wao na wanakuwa sehemu ya timu yetu ya taifa,” alihitimisha Waziri Gekul.
Ligi ya Muungano ilikuwa ikihusisha jumla ya timu sita, tatu kutoka Bara na nyingine kutoka Zanzibar ambapo katika miaka 21 ya kudumu kwa ligi hiyo ilizishuhudia Tanzania Prisons, KMKM, Majimaji, African Sports, Pan African, Malindi, Pamba, Simba na Yanga zikitwaa taji hilo kwa nyakati tofauti.
Soka Ligi ya Muungano yaundiwa mkakati
Ligi ya Muungano yaundiwa mkakati
Related posts
Read also