Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Neymar sasa ameingia katika rekodi ya wafungaji wenye mabao mengi katika historia ya klabu hiyo akishika nafasi ya nne baada ya kufunga bao lililoiwezesha timu hiyo kutoka na ushindi wa bao 1-0 Jumamosi hii dhidi ya Brest.
Hilo linakuwa ni bao la 110 kwa mshambuliaji huyo Mbrazil katika klabu ya PSG na sasa anakuwa amemzidi mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo na timu ya Taifa ya Ureno, Pauleta katika orodha ya historia ya washambuliaji wa timu hiyo wenye mabao mengi. Kylian Mbappe ndiye anayeongoza katika orodha hiyo akiwa na jumla ya mabao 180 akifuatiwa na Zlatan Ibrahimovic mwenye mabao 156.
Brest hata hivyo itabidi wajilaumu kwa kukosa penalti iliyotolewa katika dakika ya 70 ya mchezo baada Presnel Kimpembe kucheza rafu lakini mkwaju uliopigwa na Islam Slimani uliokolewa na kipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma na hivyo kuifanya PSG kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi msimu huu.
Neymar alifunga bao hilo dakika ya 30 akiitumia vizuri pasi ya Lionell Messi na sasa anakuwa amefikisha jumla ya mabao manane katika mechi saba za Ligi 1 msimu huu.
Kwa Neymar mwenye umri wa miaka 30 sasa, rekodi hiyo ina maana kubwa hasa kwa kuzingatia habari zinazoenea kwamba hana mahusiano mazuri na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, Mbappe lakini pia kabla ya kuanza msimu alinukuliwa akisema kwamba haijui hatma yake katika klabu hiyo na iliwahi kudaiwa kwamba PSG ilikuwa inajipanga kumpiga bei.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa Jumamosi hii, Marseille iliilaza Lille kwa mabao 2-1.
Kimataifa Neymar aweka rekodi PSG
Neymar aweka rekodi PSG
Related posts
Read also