London, England
Klabu ya soka ya Chelsea imeamua kumtupia virago kocha wake mkuu Thomas Tuchel hatua ambayo imechukuliwa kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo pamoja na matukio yasiyopendeza ya kocha huyo.
Uamuzi huo umechukuliwa na mmiliki mpya wa klabu hiyo, Todd Boehly ambaye katika taarifa iliyopatikana leo ilieleza kuwa mmiliki huyo na wenzake wenye hisa nyingi wanaamini huu ni wakati sahihi wa kumtafuta kocha mkuu mpya.
Jana Jumanne usiku Chelsea ilichezea kipigo cha bao 1-0 katika mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dinamo Zagreb na hivyo kuzidisha hasira walizokuwa nazo wamiliki kuhusu matokeo mabaya ya timu yao hicho kikiwa ni kipigo cha tatu msimu huu.
Tayari majina makubwa na maarufu ya makocha yameanza kuhusishwa na timu hiyo wakiwamo makocha wa zamani wa PSG, Mauricio Pochettino, Zinedine Zidane aliyekuwa akiinoa Real Madrid na wengineo.
Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England ikianza vibaya ligi hiyo kwani hadi sasa imeshinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mbili matokeo ambayo hayajawafurahisha mabosi wa klabu hiyo ambao wametoa fedha nyingi za usajili wakiamini timu hiyo itakuwa na mafanikio.
Nje ya matokeo mabaya, Tuchel pia amekuwa na mambo yasiyoridhisha ikiwamo kupigwa faini mara mbili kutokana na tabia zake zisizoridhisha jambo ambalo huenda limezidisha hasira za matajiri wake ambao tayari wametumia fedha ningi zilizotumika pamoja na mambo mengine kusajili wachezaji wapya.
Kocha huyo Mjerumani pia inadaiwa hivi karibuni alianza kushindwa kuongoza wachezaji na hakuwa na mahusiano na wachezaji hao pamoja na wajumbe wa bodi.
Hatua ya kumtimua kocha huyo imekuja wakati wamiliki wapya wa Chelsea wakifikisha siku 100 tangu waichukue timu hiyo kutoka kwa bilionea wa Urusi, Roman Abramovich.
Kimataifa Tuchel atupiwa virago Chelsea
Tuchel atupiwa virago Chelsea
Read also
