Milan, Italia
Kiungo wa Juventus na timu ya Taifa ya Ufaransa, Paul Pogba anatarajia kufanyiwa upasuaji wa goti na hivyo huenda akakosa kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Doha, Qatar, Novemba mwaka huu.
Poga mwenye umri wa miaka 29, aliumia Julai mwaka huu hali ambayo imemnyima nafasi ya kuiwakilisha Juventus msimu huu na awali ilitarajiwa angekuwa fiti kwa ajili ya kuiwakilisha Ufaransa kwenye Kombe la Dunia.
“Asubuhi ya leo, Pogba amefanya mazoezi kwa mara ya pili lakini akaacha na baadaye ikaamuliwa anahitaji kufanyiwa upasuaji, kimsingi tunatarajia awe tayari kwa kucheza kuanzia mwezi Januari” alisema kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri.
Ligi Kuu Italia au Serie A itasimama baada ya mechi za Novemba 13 kwa ajili ya kupisha fainali za Kombe la Dunia na kuanza tena Januari wakati Ufaransa inatarajia kuanza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Australia itakayopigwa Novemba 22.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Pogba kukosa mechi za fainali za Kombe la Dunia, Allegri alisema, “Kombe la Dunia si tatizo letu, tatizo tulilonalo Juventus ni kwamba Pogba hatutakuwa naye hadi mwezi Januari.”
Pogba alijiunga na Juventus majira ya kiangazi msimu huu baada ya mkataba wake na Man Utd kufikia ukomo na klabu hiyo kutoonyesha utayari wa kumuongezea mkataba mpya.
Kimataifa Pogba hatihati Kombe la Dunia
Pogba hatihati Kombe la Dunia
Related posts
Read also