Na mwandishi wetu
Bondia wa Tanzania, Hassan Mwakinyo maarufu ‘Champez’ kesho Jumamosi hii usiku atapanda ulingoni kuzichapa na Liam Smith raia wa England kwenye pambano la ubingwa wa dunia katika uzito wa super-welter jijini Liverpool, England.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ngumi hapa nchini, England na kwingineko duniani litakuwa la raundi 12 na litafanyika kwenye Ukumbi wa M&S Bank Arena ambako kwa saa za Afrika Mashariki litaonyeshwa kuanzia saa 3.00 za usiku.
Kwa Mwakinyo hili linakuwa pambano lake la kwanza tangu alipopigana mara ya mwisho Septemba mwaka jana na kumtandika Julius Indongo kwa ushindi wa TKO na hivyo kufanikiwa kuutetea ubingwa wa Afrika (ABU).
Hata hivyo kwenye ardhi ya England, Mwakinyo ndipo mahala alipotangaza ubabe wake baada ya kumtwanga bondia namba nane wa dunia wakati huo, Sam Eggington mwaka 2008 na Mwakinyo kupanda mpaka nafasi ya 14 kabla ya kuporomoka mpaka nafasi ya 40 akiwa na nyota tatu na nusu kutokana na kutopanda ulingoni kwa zaidi ya miezi 10.
Upande wa Liam anayeshika nafasi ya sita, yeye aliutetea mkanda wake huo wanaoupambania leo mnamo Aprili, mwaka huu kwa kumchapa Jessie Vargas kwenye Ukumbi wa Madison Square, New York.
“Mwakinyo si mpiganaji mbaya. Alikuja, akamshinda Sam Eggington na hajashindwa tangu wakati huo lakini kwa heshima zote, mimi si Sam. Mwakinyo ni mtu hatari, anacheza sana ulingoni na ana mikono mizito na katika kiwango hicho, napaswa kubadilika kuwa katika mlengo kama huo,” alisema Liam.
“Cha kufurahisha zaidi, alifunzwa na makocha wangu, Joe McNally na Declan O’Rourke kwa mapambano yake mawili. Nina hofu kidogo ndani yangu lakini nafikiri nitakuwa mzuri zaidi ya Hassan, najiamini katika uwezo wangu, naaamini nitakamilisha kazi yangu vizuri,” alisema Liam juzi alipokuwa akihojiwa kuhusu pambano hilo.
Mwakinyo anayejifua Florida nchini Marekani kwa sasa hivi, aalikaririwa hivi karibuni akieleza kwa kifupi anavyoutamani usiku wa pambano hilo: “Mara kadhaa najiwa na ari sana kila nikitafakari juu ya usiku ambao nitatangazwa rasmi kuwa bingwa wa WBO, rasmi kutoka Tanzania, Tanga Makorora, dah!”
Ngumi Hukumu ya Mwakinyo Jumamosi usiku
Hukumu ya Mwakinyo Jumamosi usiku
Read also
