Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amewaeleza wazi wachezaji wa kikosi hicho kutowadharau wapinzani wao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Zolan FC kutoka Sudan Kusini wakidhani kwamba ni timu dhaifu.
Yanga itaanza kampeni ya michuano hiyo kwa kukabiliana na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Sudan Kusini huku mechi zote mbili zikitarajiwa kuchezwa Tanzania, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikielezwa kuwa hali ya usalama nchini kwao si nzuri.
Mbali na hilo, timu hiyo inaonekana dhaifu kwa kushindwa kuhimili mambo mengi kiuchumi kulingana na picha za maandalizi, mechi na hata usafiri wanaoutumia kuelekea kwenye mechi zao.
Akizungumza na GreeenSports, kocha huyo ameeleza kuwa yeye na bosi wake Nasreddine Nabi, wamekuwa wakizungumza na wachezaji wao kila baada ya mazoezi, kuwasihi kutowadharau Zolan kwa sababu kwenye mpira chochote kinatokea.
“Watu wengi wanaipa nafasi ya kusonga mbele Yanga kutokana na udhaifu wa wapinzani, nani anaijua ligi ya Sudan Kusini? Sheria za mchezo wa soka zinataka umheshimu mpinzani bila kujali mazingira aliyokuwa nayo na sisi pia tumewaambia wachezaji kuacha kusikiliza maneno ya watu mtaani tunapaswa kuwaheshimu na kucheza kwa malengo,” alisema Kaze.
Kocha huyo alisema kuanza kuwaza mchezo unaofuata dhidi ya St. George au Al Hilal ni makosa makubwa kwani ikitokea wanafungwa na Zolan ni wazi kuwa hawatokutana na timu hizo ambazo watakutana na mojawapo baada ya kuruka kiunzi cha Zolan.
Msimu uliopita katika michuano hiyo, Yanga ilitolewa kwenye hatua ya awali na Rivers United ya Nigeria, jambo ambalo viongozi wa timu hiyo hawataki kuona likijirudia msimu huu.
Soka Kaze ataka Yanga wasiidharau Zolan FC
Kaze ataka Yanga wasiidharau Zolan FC
Related posts
Read also