Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imeeleza kutambua ugumu wa mchezo wao dhidi ya Yanga kutokana na ubora wao lakini wametamba kuwa wanahitaji pointi tatu ili kujiweka mapema karibu na ubingwa msimu huu.
Azam imefafanua kuwa ingawa msimu uliopita hawakuambulia pointi dhidi ya Yanga lakini hayo ni mambo yaliyopita na sasa wanaangalia namna gani wataibuka na ushindi watakapoumana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Septemba 6, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria alisema wanauangalia mchezo huo kwa lengo la kupata matokeo hasa ukizingatia kwenye mechi yao ya mwisho hawakupata ushindi, hivyo wanahitaji kuweka mambo sawa kwenye mechi hiyo.
Katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu, Azam ilitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita wakati mechi ya kwanza waliifunga Kagera Sugar mabao 2-1.
“Tunaongelea mchezo huu kama mchezo mpya na tutaingia kwa lengo la kupata matokeo mazuri, mchezo uliopita wa ligi hatukufanya vizuri, hatukushinda, hatukupata pointi tatu kwa hiyo tusipopata tena pointi katika mechi hii tutazidi kujiweka mbali na ubingwa ambao tunautaka kweli kweli msimu huu.
“Kwa hiyo tutaingia tukiwaheshimu Yanga, mabingwa watetezi, hawajapoteza mchezo muda mrefu sana, wameshasahau machungu hayo, sasa tukipata nafasi ya kuwapa machungu itakuwa jambo zuri, timu yao iko vizuri sana kila eneo lakini mpira ni mpango kwahiyo mpango wa kocha alioutengeneza kwa ajili ya mechi unaweza kutupa matokeo kama mambo yataenda vizuri,” alisema.
Azam itaingia dimbani ikiwa inashikilia nafasi ya tano kwa pointi nne wakati Yanga ikiwa nafasi ya pili kwa pointi sita sawa na vinara Simba waliokaa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Soka Azam: Mechi na Yanga ngumu lakini…
Azam: Mechi na Yanga ngumu lakini…
Related posts
Read also