Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mecky Maxime ameanza kuipigia hesabu mechi yao na timu ya Taifa ya Uganda au Uganda Cranes akisema kwamba ingawa soka ni mchezo usiotabirika lakini watajitahidi kuanza kazi yao vizuri kwa kupata matokeo.
Maxime nahodha wa zamani wa Stars na timu ya Mtibwa Sugar, mbali na kuizungumzia mechi hiyo ya marudiano na Uganda Cranes pia ameshukurun kwa kupewa nafasi hiyo kulipigania taifa lake huku akisisitiza ushirikiano kwa Watanzania wote katika kuipeleka nchi ya ahadi timu hiyo.
“Hakuna asiyetamani kupata nafasi hii maana hii ni timu yetu wote Watanzania kwa hiyo kikubwa ni kushirikiana. Mchezo wa soka ukiwa kama kocha ni kama unacheza kamari wakati mwingine, ni kama unafanya ‘sub’ ya mchezaji na huwezi kujua kama ataenda kuleta unachotaka au atakosea,” alisema kocha huyo mpya wa Stars.
“Kwa hiyo siwezi kusema maneno mengi sana kikubwa ni kufanya kazi, mpira ni mchezo wa wazi kila mtu anauona kwa hiyo kazi yetu itaonekana kutokana na matokeo yatakayopatikana,” alieleza Maxime.
Kuhusu mchezo huo wa marudiano ambao ni wa kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani au CHAN utakaopigwa Septemba 3, mwaka huu nchini Uganda, kocha huyo alisema inawezekana kupata matokeo dhidi ya Uganda ingawa itawabidi kupambana.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Stars ililala kwa bao 1-0 na kupelekea kuondolewa kwa kocha Kim Poulsen na mikoba yake kupewa Mzambia, Hanour Janza akisaidiwa na Maxime na kocha wa makipa, Juma Kaseja.
“Huu ni mchezo wa mpira tusidanganyane, kikubwa tumepewa nafasi acha tufanye kile tunachoweza kwa mechi hii lakini nafikiri mbele huko yatakuwepo makubwa zaidi, kwa hiyo mechi hii acha tukapambane tutafute matokeo na inawezekana sio kama haiwezekani, inawezekana vizuri tu.
“Kama nilivyosema tushirikiane, tunaweza kufanya kazi lakini kwanza kuombeana uzima na wao pia mashabiki wana mchango mkubwa, warudi tuipende timu yetu, hilo ndiyo muhimu zaidi kuliko mimi kuja hapa. Watanzania tuje uwanjani wachezaji nao wapate moyo, tuipende timu yetu tuwatie moyo wachezaji wetu,” alisisitiza Maxime.
Kimataifa Maxime aipigia hesabu Uganda Cranes
Maxime aipigia hesabu Uganda Cranes
Read also
