Manchester, England
Baada ya Cristiano Ronaldo kuanzia benchi katika mechi dhidi ya Liverpool jana, kocha wa Man Utd, Eric ten Hag amempoza mchezaji huyo akisema bado ana nafasi katika timu yake na atamfaa katika mfumo atakaoutumia.
Kauli hiyo imekuja wakati huu majaliwa ya mchezaji huyo yakiwa kwenye utata kwani licha ya kudai anataka kuondoka, kuanzia benchi kwenye mechi muhimu dhidi ya Liverpool ambayo Man Utd ilishinda kwa mabao 2-1 kumetafsiriwa na wengi kuwa huenda Ten Hag ameanza kumfungulia mchezaji huyo mlango wa kutokea.
Muunganiko wa Jadon Sancho na Marcus Rashford pamoja na Anthony Elanga umeonekana kuwa na maana katika mechi na Liverpool na hivyo kuonekana kuwa ni mwanzo wa kuachana na Ronaldo lakini Ten Hag amepinga hilo akidai kwamba anaweza kumjumuisha mchezaji huyo katika mfumo wake.
“Nafikiri anaweza kufaa, katika maisha yake yote ya soka amekuwa na makocha tofauti, amefaa katika mifumo tofauti, wakati wote ameonyesha uwezo, kwa nini isiwe sasa,” alisema Ten Hag ambaye katika mechi hiyo alimpa nafasi Ronaldo dakika nne kabla ya mpira kumalizika akiingia badala ya Rashford.
“Suala la umri wake si tatizo, kama wewe una uwezo na una umri mkubwa na bado unacheza kwa kiwango kizuri ni kwamba wewe uko vizuri kiasi cha kutosha,” alisisitiza Ten Hag.
Baada ya kipigo cha mabao 4-0 ambacho Man Utd ilikipata kwa Brentford juma lililopita, Ronaldo akawa mmoja wachezaji wanne waliohusika katika mabadiliko yaliyofanywa na Ten Hag katika mechi na Liverpool, wengine ni nahodha Harry Maguire, Luke Shaw na Fred ambao pia walisugua benchi.
“Tuna kikosi na tuna namna ya uchezaji, lakini pia tunakuwa na mpango wa mechi husika, unaangalia mbinu ipi bora ya kuingia nayo kiuchezaji, tunahitaji kuwa na kikosi kwa sababu tuna mechi nyingi za kucheza, tunakuwa pamoja kama timu na hapo tutafanikiwa kwa mengi, naamini hivyo,” alisema Ten Hag alipoulizwa swali kuhusu nini hasa alichozingatia wakati akipanga kikosi cha kuivaa Liverpool.
Kimataifa Ten Hag ampoza Ronaldo
Ten Hag ampoza Ronaldo
Related posts
Read also