Manchester, England
Hatimaye klabu ya Manchester United imefanikisha mpango wa kumsajili kiungo wa Real Madrid, Casemiro baada ya klabu hizo mbili kufikia makubaliano kwa ada inayofikia Pauni 60 milioni.
Kufikia makubaliano kwa klabu hizo mbili maana yake ni kwamba Casemiro sasa anajiandaa wakati wowote kuachana na Ligi Kuu Hispania (La Liga) na kuanza kukipiga katika Ligi Kuu England mara baada ya kukamilisha vipimo vya afya na kupata kibali cha kufanya kazi Uingereza.
Klabu zote mbili zimethibitisha hilo ambapo mchezaji huyo anatarajia kusaini mkataba wa miaka minne ambao pia una kipengele kinachompa nafasi ya kuongeza mwaka mmoja.
“Real Madrid inapenda kumshukuru Casemiro, mchezaji ambaye ni sehemu ya wakongwe wa klabu hii, tangu ajiunge na timu hii Januari 2013 akiwa na miaka 20 amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika moja ya zama za mafanikio katika historia ya klabu yetu, ni mchezaji wa mfano aliyejitolea kwa kila hali kwa ajili ya Real Madrid, Real Madrid ni nyumbani kwake na itabaki kuwa hivyo siku zote,” ilieleza taarifa ya Real Madrid.
Usajili wa Casemiro unaweza kuwa mwanzo wa mafanikio kwa Man Utd ambayo imekuwa ikisaka kiungo, awali ilikuwa ikimtaka kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong lakini kadri siku zinavyokwenda mpango huo unaonekana kushindikana baada ya mchezaji huyo kuamua kubaki Barcelona ndipo Man Utd walipohamishia akili zao kwa Casemiro.
Casemiro ambaye ni Mbrizil, inadaiwa awali alikataa kujiunga Man Utd lakini nguvu ya pesa inadaiwa kumfanya ashawishike kubadili mawazo baada ya kutangaziwa mshahara mkubwa kuliko ambao amekuwa akiupata Real Madrid na sasa anatarajia kuwa mmoja wa wachezaji wa Man Utd wanaolipwa mshahara mkubwa.
Sambamba na hilo usajili wa Aurelien Tchouameni katika klabu ya Real Madrid unazidi kuongeza ushindani katika nafasi ya kiungo na hiyo pia inatajwa kuwa sababu mojawapo iliyomshawishi Casemirio kuwa tayari kuondoka katika klabu hiyo.
Uamuzi wa Casemiro kuondoka, Real Madrid aliufikia Ijumaa asubuhi akiwa mazoezini mbele ya kocha wake, Carlo Ancelotti ambaye ndiye aliyethibitisha kwamba kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 alimwambia kwamba anataka kuondoka katika klabu hiyo.
“Tumezungumza asubuhi, anataka kujaribu changamoto mpya, fursa mpya na kwa hilo nimemuelewa, kwa kile alichokifanya kwa klabu hii na kwa timu hii, hakika tunahitaji kumpa heshima yake,” alisema Ancelotti.
Kimataifa Casemiro sasa mali ya Man Utd
Casemiro sasa mali ya Man Utd
Related posts
Read also