Manchester, England
Winga wa Manchester United, Cristiano Ronaldo amesema kwamba ana kitabu maalum chenye mambo aliyoyaita ya uwongo ambayo yamekuwa yakiandikwa na kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari kuhusu majaliwa yake katika klabu hiyo na kumhusisha na mipango ya kuhama.
Ronaldo amekuwa gumzo katika siku za karibuni huku kukiwa na utata kuhusu kinachodaiwa kuwa ni nia yake ya kutaka kuihama Man Utd ili apate nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mwaka mmoja tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Juventus.
Pamoja na uvumi wote huo mabosi wa Man Utd hususan kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag wamekuwa wakisisitiza kwamba winga huyo mwenye umri wa miaka 37 hauzwi na tayari klabu za Bayern Munich, Atletico Madrid na Chelsea zilizokuwa zikihusishwa na mipango ya kutaka kumsajili, nazo kwa nyakati tofauti zimetangaza kujiweka kando na mpango huo.
Wakati yote hayo yakiendelea, Ronaldo akitumia mitandao ya kijamii amevituhumu vyombo vya habari kwa kusema uwongo na kwamba ni habari chache mno zenye ukweli kati ya nyingi ambazo zimekuwa zikitoka kwenye vyombo vya habari kumhusu yeye.
“Wanaujua ukweli baada ya kufanya mahojiano katika wiki kadhaa, vyombo vya habari vinasema uwongo, nina kijitabu cha kumbukumbu, katika miezi michache, kati ya habari 100 zilizonihusu, ni tano tu zenye ukweli, fikiria hali hiyo,” alisema.
Hata hivyo nahodha wa zamani wa Man Utd, Gary Neville ameibuka na kumsema Ronaldo akimtaka kuonyesha ukomavu wa kiuongozi katika wakati mgumu ambao klabu hiyo inapitia. “Ni kwa nini mchezaj bora wa wakati wote (kwa maoni yangu) analazimika kusubiri wiki kadhaa zipite ndipo awaambie ukweli mashabiki wa Manchester United?” Alihoji Neville.
“Simama na uzungumze, klabu inapitia wakati mgumu na inahitaji viongozi wa kuweka sawa mambo, yeye ni mtu pekee anayewea kuikabili hali ilivyo sasa,” alisema Neville.
Ronaldo hakushiriki ziara za timu hiyo za maandalizi ya msimu wa 2022/23 katika nchi za Thailand na Australia na akaibuka mara ya kwanza kwenye mechi moja ya kirafiki, baada ya hapo akakosa mechi ya kwanza ya timu hiyo ya Ligi Kuu England lakini akacheza mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo ambayo ni ya pili kwa timu yake wiki iliyopita, mechi ambayo Man Utd ilibugizwa mabao 4-0 na Brentford.
Kimataifa Ronaldo adai waandishi waongo
Ronaldo adai waandishi waongo
Related posts
Read also