Paris, Ufaransa
Kwa mara ya kwanza mchezaji nyota, Lionel Messi ameachwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Ballon d’Or ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu mwaka 2005.
Messi hayumo katika orodha ya wachezaji 30 iliyotolewa Ijumaa hii na France Football ambapo mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema anaongoza orodha hiyo akiwania kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza akibebwa na mafanikio ambayo ameyapata kwa msimu wa 2021/22.
Messi jina lake limekuwapo katika orodha ya kuwania tuzo hiyo kwa miaka 15 mfululizo akiwa ameshinda mara saba kati ya hizo, kukosekana kwake kwa kiasi kikubwa kumetokana na msimu mbaya aliokuwa nao katika klabu ya PSG ya Ufaransa aliyojiunga nayo akitokea Barcelona.
Kama ilivyo kwa Messi nyota mwenzake wa PSG, Neymar naye hayumo katika orodha hiyo wakati jina la Cristiano Ronaldo wa Man United limo kama ilivyo kwa Robert Lewandowski wa Barcelona, Erling Haaland wa Man City pamoja na mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah.
Orodha kamili ya wachezaji hao ni kama ifuatavyo…Trent Alexander-Arnold, Benzema, Joao Cancelo Casemiro, Thibaut Courtois, Ronaldo, Kevin De Bruyne, Luis Diaz, Fabinho, Phil Foden, Erling Haaland, Sebastian Haller, Harry Kane, Joshua Kimmich na Rafael Leao.
Wengine ni Lewandowski, Riyad Mahrez, Mike Maignan, Sadio Mane, Kylian Mbappe, Luka Modric,
Christopher Nkunku, Darwin Nunez, Antonio Rudiger, Mohamed Salah, Bernardo Silva, Son Heung-min,
Virgil van Dijk, Vinicius Jr na Dusan Vlahovic.
Kwa upande wa wanawake, wachezaji watatu wa timu ya Taifa ya wanawake ya Marekani, Catarina Macario, Alex Morgan na Trinity Rodman majina yao yamo katika orodha ya wachezaji 20 wanaowania tuzo hiyo.
Kinara wa mwaka jana wa tuzo hizo, Alexia Putellas naye ni miongoni mwa wachezaji wanawake watano wa klabu ya Barcelona ambao majina yao yamo kwenye orodha hiyo kama ilivyo kwa wachezaji watatu wa timu ya Taifa ya England, Millie Bright, Lucy Bronze na Beth Mead ambao walikuwa na mchango mkubwa kwa timu ya England hadi kutwaa taji la Ulaya. Tuzo hizo zinatarajia kutolewa Oktoba mwaka huu.
Soka Messi hayumo Ballon d’Or
Messi hayumo Ballon d’Or
Read also