Manchester, England
Winga wa zamani wa Man Utd, Ryan Giggs amefikishwa mahakamani mjini Manchester kwa tuhuma kadhaa ikiwamo kumpiga kichwa mpenzi wake wa zamani, Kate Greville huku pia akidaiwa kuwa mwenye tabia ya kupenda ngono mara kwa mara.
Giggs anadaiwa kufanya kitendo hicho Novemba Mosi, 2020 baada ya wawili hao kukorofishana ambapo alimshika Kate mabegani kisha akamuangalia usoni, kabla ya kumpiga kichwa.
Katika tukio jingine la ubabe wa Giggs inadaiwa wawili hao walikuwa wakigombea simu baada ya Kate kuiweka simu ya Giggs chumba kingine jambo lililomkera Giggs na akaamua kuichukua simu ya Kate ndipo walipoanza kugombea simu hiyo kabla Giggs hajamlaza chini na kumkaba kisha kuchukua simu hiyo na kuondoka zake wakati wote huo Kate alikuwa akilia kuomba msaada.
Kate pia aliiambia mahakama kwamba Giggs alikuwa akitaka kufanya ngono kila wakati, na wakati mwingine alikuwa akimtumia hovyo ujumbe mfupi na picha zenye maudhui ya ngono kwenye simu
“Hakika haukuwa wakati mzuri kwangu, nilijiona kama mtu ninayetumiwa kumridhisha kwa mahitaji yake ya ngono, haijawahi kutokea wakati asiwe mwenye uhitaji wa ngono.
“Baba yangu aliwahi kumwambia anaumwa saratani, lakini hakuiangalia hata simu, badala yake wakati wote alikuwa akiniambia ninamkera, huku akiniambia niondoke.”
Giggs katika tuhuma nyingine anadaiwa alikuwa akimkera Kate kwa kumwambia yuko kama Stacey Cooke, mke wa zamani wa Giggs ambaye ni mama wa watoto wake wawili na ambaye wameachana sababu kubwa ikidaiwa kuwa ni tabia za Giggs za ubabe na kutotaka kupingwa.

“Alikuwa akinishambulia kwa kuniambia niko kama Stacey ambaye alidai kwamba alikuwa na tatizo la ulevi na aliyafanya maisha yake kuwa ya matatizo, na kuna wakati aliniita kwa jina la Stacey,” alisema Kate.
Kate aliiambia mahakama kwamba kuna wakati alijaribu kumkwepa Giggs kwa kwenda Abu Dhabi na baadaye Dubai na hakuamini kama Giggs angeweza kumkimbia mke wake kwa ajili ya kuwa na yeye,
“Niliamua kumkimbia na kwenda kuishi Dubai, niliona mahusiano haya hayakuwa mazuri kwangu, niliona aibu kwani alikuwa ni mume wa mtu na sikutaka mtu yeyote afahamu.
“Katika hali ya kawaida nilijikuta nikivurugwa na mapenzi yake, alikuwa akinifukuzia na kunitumia ujumbe mfupi, alinishawishi, kuna mambo mengine niliyasikia kuhusu yeye lakini aliyapinga, hali ilikuwa hivyo kwa muda mrefu.
Baada ya vyombo vya habari kujua habari yake na Giggs, Kate aliamua kum-block Giggs lakini ikawa balaa, “kukawa na ujumbe wa email mara kwa mara, niliamua bora iwe tu, nikaanza kuzungumza naye tena.”
Wakiwa pamoja, Kate akajikuta akipewa habari za Giggs kwamba yote aliyokuwa akimwambia ilikuwa kama ahadi tu lakini baadaye watu walikuwa wakimpa za ndani kuhusu Giggs kuhusu mambo ambayo ameonekana akiyafanya.
“Ilikuwa kama watu wawili tofauti, kati ya mtu ambaye aliniambia alivyo na mtu ambaye nilisikia habari zake kwa watu, sikujua niamini kipi, je alikuwa mtu mzuri au mbaya, alikuwa akiniambia ukweli au alikuwa akinidanganya? Nilikaa chini na kujiona kama mtu aliyekuwa akikimbia marathon na kuchoka hadi kushindwa kupumua,” alisema Kate.
Kate pia aliiambia mahakama kwamba Giggs aliwahi kumtumia mke wa mtu picha yake akiwa mtupu na alilijua hilo baada ya mtu mmoja, mume wa huyo mwanamke kumtumia Kate email iliyoambatanishwa na picha ya mtu mwanaume aliyekuwa mtupu akimuuliza kama mtu huyo ni Giggs au la.
Kate aliiambia mahakama kwamba siku ya tukio hilo alikuwa na Giggs Dubai na siku moja kabla Giggs alikuwa katika mzozo kwenye simu kwa dakika 20 wakati huo wakiwa wanapata chakula cha jioni na hapo hapo mtu huyo akasema kwamba asingependa jambo hilo lijulikane kwa kuwa yeye ana watoto.
Baadaye Kate alimfuata Giggs na kumwambia kuhusu jambo hilo, kwanza alibisha hadi alipoangalia kwenye simu na kuona ushahidi kwamba alimtumia mwanamke huyo picha hiyo wiki mbili zilizopita, “Hakuweza kubisha kwa sababu nilikuwa na ushahidi, badala yake akawa mtu mzuri kweli kwangu, Ryan mzuri niliyekuwa naye mwanzo, hata hivyo hali hiyo ilikuwa ya muda mfupi tu, akarudi katika uhalisia wake taratibu.”
Katika tuhuma nyingine, Giggs anadaiwa kumtumia video za ngono Kate huku akimtisha na kumwambia kwamba hataki tena kufanya naye kazi na kwamba anachotakiwa ni kumjibu ujumbe huo au kum-block asipofanya hivyo angewasiliana na bosi wake na kumwambia kwamba hayo ndiyo mambo anayofanya kazini.
Kate anasema kwamba hakutaka hata kuziangalia video hizo, alizifuta haraka, “zinaweza kuwa za kuchekesha lakini zimejaa maudhui ya ngono, niliogopa angeniharibia kazini, nilihisi angeweza hata kutumia email za ofisini kutuma picha hizo.”.
Kate pia aliiambia mahakama kwamba Giggs alikuwa akimlaghai kwenye mahusiano yao kwani alikuwa akijirusha na wanawake wengine wanane tofauti, mambo ambayo Kate aliyabaini baada ya kufungua iPad ya Giggs. “Uhalisia niliokutana nao kwenye iPad ilikuwa ni tukio baya kuliko hata nilivyokuwa nikidhani.
Kate alimtaja mmoja wa wanawake hao kwa jina la Helen ambaye alisafiri na Giggs ndege moja wakati Giggs akielekea Barcelona kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mwingine alimtaja kwa jina la Zara ambaye alibaini hilo wakati wakielekea Urusi kwenye mechi za Kombe la Dunia 2018.
Katika tuhuma nyingine, Kate alisema kwamba Giggs alikuwa akimpiga mara kwa mara mfano ni siku ambayo alimgaragaza chini wakiwa kwenye chumba cha hoteli na kumkamata kiunoni kwa nguvu na kuanza kumvuta sakafuni wakati huo Kate akiwa amevaa taulo kabla ya kutupa vitu vyake kwenye varanda nje ya chumba walichofikia, hilo likiwa tukio la kwanza la ukatili kufanyiwa na Giggs.
Katika tukio jingine, wakiwa kitandani, Giggs alianza kumpiga mgongoni na kumfanya aanguke, akiwa chini Giggs alichukua laptop na kumpiga nayo kichwani na kumuacha akiwa na majeraha.
Siku nyingine, Giggs alidaiwa kuuvuta kwa nguvu mkoba aliokuwa ameushikilia Kate hadi Kate akaanguka chini, dada yake Kate, Emma alipoingilia kati Giggs alimpiga mdomoni kwa kiwiko.
Giggs ambaye ameichezea kwa mafanikio klabu ya Man Utd, hivi karibuni alitangaza kujiuzulu kuinoa timu ya Taifa ya Wales kwa alichodai kwamba asingependa tuhuma zinazomkabili ambazo tayari amezikana, ziathiri kwa namna yoyote maandalizi ya Wales kwenye fainali za Kombe la Dunia.