London, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema kipigo cha mabao 2-1 walichokipata mbele ya Brighton kimetokana na wachezaji kutojiamini na kusumbuliwa na matokeo mabaya ya msimu mbaya uliopita.
Man United leo imeshindwa kutamba katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England ambayo pia ni ya kwanza kwa kocha Ten Hag ambaye amejiunga na timu hiyo akitokea Ajax ya Uholanzi. Hadi mapumziko, Brighton walikuwa mbele kwa mabao ya Pascal Gross kabla ya Man United kupata bao pekee katika dakika ya 68 ambalo Mac Allister alijifunga.
“Nafikiri mwanzo ulikuwa mzuri lakini baada ya hapo tulianguka katika kujiamini na kuanza kufanya makosa na wapinzani wetu wakatuadhibu katika hilo,” alisema Ten Hag mara baada ya mechi hiyo.
“Nashindwa kuielewa hiyo hali ya kukosa kujiamini baada ya msimu uliopita lakini hilo si muhimu, hawa ni wachezaji wazuri,” alisema.
“Nilijua hali hiyo ingeweza kujitokeza lakini tungeweza kufanya vizuri hilo liko wazi ingawa mabadiliko hayaji kwa ghafla, leo hatukua wazuri kwenye kipindi cha kwanza na ni lazima tujifunze kutokana na hilo, jambo hilo nalo lipo wazi.”
Katika mechi hiyo Ten Hag alimuweka benchi Cristiano Ronaldo badala yake alimpa nafasi mchezaji wake mpya Christian Eriksen ambaye alimchezesha kama namba tisa feki licha ya matarajio makubwa ya awali kwamba Ronaldo angecheza hasa baada ya kuumia kwa Anthony Martial.
Ten Hag hata hivyo alitetea uamuzi wa kutomchezesha Ronaldo akisema, “kama kungekuwa na mshambuliaji ningeweza kumchezesha, kwa sasa Ronaldo labda anahitaji siku 10 katika mazoezi ya timu na dakika 90 zitamsumbua, kwa hiyo ndio sababu hatukumchezesha.”
Wakati mambo yakiwa mabaya kwa Man United, majirani zao wa City walikuwa na furaha katika mechi yao ya kwanza ya ligi hiyo baada ya kuichapa West Ham mabao 2-0, kinara wa mabao hayo akiwa ni mshambuliaji wao mpya, Erling Haaland aliyefunga katika dakika za 36 (kwa penalti) na dakika ya 65. Nao Leicester na Brentford waliishia kugawana pointi moja moja baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.
Kimataifa Ten Hag alaumu wachezaji kwa kipigo
Ten Hag alaumu wachezaji kwa kipigo
Read also