Paris, Ufaransa
Bao la tikitaka au bicycle-kick kama wanavyoita Wazungu, ndilo ambalo Lionel Messi ameifungia PSG Jumamosi hii wakati timu hiyo ikitoka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Clermont katika mechi yao ya kwanza ya Ligi I nchini Ufaransa.
Ushindi huo ni mwanzo mzuri wa PSG katika kulitetea taji la Ligi 1 na unazidi kuibua ari kwa timu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa mafanikio inayoyapata hayaendani na uwekezaji uliofanywa katika timu hasa baada ya kutolewa mapema hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita wa 2021/22.
Huo ni ushindi mnono wa pili kwa timu hiyo katika kipindi kisichozidi siku saba baada ya wikiendi iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Nantes katika mechi ya kuwania taji la Des Champions ambalo ni sawa taji la Ngao ya Jamii.
Mbali na Messi ambaye alifunga mabao mawili, mabao mengine yalifungwa na nyota mwenzake wa zamani wa Barcelona, Neymar aliyefungua ukurasa wa mabao kwa timu hiyo katika dakika ya tisa akifuatiwa na Achraf Hakimi katika dakika ya 26 na Marquinhos dakika ya 38 kabla Messi hajamalizia mabao yake mawili katika dakika za 80 na 86.
Kati ya mabao yote hayo ya PSG, bao la Messi alilofunga dakika ya 86 limeendelea kuwa katika kumbukumbu za mashabiki kutokana na ubora wake, mchezaji huyo baada ya kuinasa pasi ya Leandro Paredes aliutuliza vizuri mpira kifuani na kupiga tikitaka iliyokwenda wavuni.
PSG katika mechi hiyo ilimkosa mshambuliaji wake nyota, Kylian Mbappe ambaye ni majeruhi lakini kocha mpya wa timu hiyo, Christophe Galtier aliwapa nafasi ya kuiwakilisha PSG katika Ligi 1 kwa mara ya kwanza wachezaji, Vitinha, Hugo Ekitike na Nordi Mukiele.
Mechi nyingine za Ligi 1 matokeo ni kama ifuatavyo…
Strasbourg 1-2 Monaco
Lyon 2-1 Ajaccio
Kimataifa Messi apiga tikitaka PSG ikiua 5-0
Messi apiga tikitaka PSG ikiua 5-0
Read also
