Na mwandishi wetu
Singida Big Stars ikionekana kuja kivingine jana iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 dhidi ya Zanaco ya Zambia katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.
Mechi hiyo iliyoandamana na tamasha la Singida Big Stars Day pia ilikuwa maalum kuukaribisha msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC wa 2022/23 ambao unaanza rasmi baadaye mwezi huu na kuwatambulisha wachezaji wao wapya watakaoiwakilisha timu hiyo.
Ushindi huo umepatikana kwa bao pekee la nyota wa zamani wa Yanga, Deus Kaseke baada ya mabeki wa Zanaco kukosa umakini katika kuokoa krosi iliyopigwa na Amissi Tambwe kabla ya mpira kumkuta mfungaji aliyefumua shuti lililojaa wavuni.
Juhudi za Zanazo kutaka kusawazisha bao hilo hazikuweza kuzaa matunda na hadi mpira unamalizika, Singida Big ambayo awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la DTB ilitoka Uwanja wa Namfua ikiwa kifua mbele huku ikiwapa matumaini makubwa mashabiki wake.
Mechi hiyo pamoja na mambo mengine imeonyesha namna ambavyo Singida Big imekuja kivingine ikitarajiwa kutoa ushindani mkali katika Ligi Kuu ya NBC, ushindani ambao dalili zake zimeanza kujionyesha jana kwa wachezaji wa Yanga, Kaseke na Tambwe kutema cheche..
Ukiachana na wachezaji hao, Singida Big pia inaye beki wa zamani wa Simba na Azam, Paschal Wawa, baada ya kuachwa na Simba mashabiki wengi waliamini kwamba huo ulikuwa mwisho wa mchezaji huyo katika soka la Tanzania lakini Singida ikaamua kumvuta kwa mara nyingine na huenda ni usajili uliofanywa na Hans Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa ndiye anayeinoa timu hiyo.
Hapo hapo, Singida ina Juma Abdul ‘Mnyamani’ ambaye katika hali isiyotarajiwa alionyesha uwezo na kutoa matumaini kama ilivyokuwa kwa Said Ndemla, mchezaji mwingine anayeongeza idadi ya wachezaji wazoefu katika kikosi cha Singida Big.
Pia tusimsahau Meddie Kagere, mshambuliaji aliyejijengea sifa akiwa Simba kabla ya kuachwa naye yumo katika kikosi cha Singida Big, kama ilivyo kwa wazoefu wengine wa Ligi Kuu ya NBC, Kagere naye yumo katika kunid la wazoefu hao ambao watataka kudhihirisha kwamba bado wana uwezo.
Timu hiyo pia imetoka nje ya mipaka ya Tanzania, ina mastaa wawili kutoka Brazil, Peterson Cruz na Dario Frederico, wote hao wanaifanya Singida Big Stars kuwa timu tofauti iliyokuja kivingine na hapana shaka itazidi kuongeza msisimko na ushindani kwenye ligi katika msimu wa 2022/23.
Kimataifa Singida Big Stars yaja kivingine
Singida Big Stars yaja kivingine
Read also
