Na mwandishi wetu
Usiku wa kuamkia leo Yanga imetangaza kumuongezea mkataba kocha wake, Nasreddine Nabi na sasa ataendelea kukinoa kikosi hicho mpaka mwaka 2024 na hivyo kufuta uvumi ulionea siku za karibuni kuhusu uwezekano wa kocha huyo kuondoka. .
Haikuhitaji kuumiza kichwa kwamba kwanini Yanga imeamua kuongeza mkataba na kocha huyo, kwa sababu ndiye aliyekuwa dereva mkuu wakati Yanga inarejea kwenye ubabe wake kwenye Ligi Kuu ya NBC Bara.
Kocha huyo ndiye aliyehusika kuisuka timu hiyo inayoimbwa kila kona leo akiipa mataji matatu, ubingwa wa ligi, Kombe la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.
Mafanikio ya Nabi hayakuishia Afrika Mashariki, taarifa zake zilisambaa kona nyingi Afrika na mwisho akaanza kuhusishwa kuwaniwa na vigogo, Wydad Casablanca na FAR Rabat wanaoelezwa kuwa walishamuandalia Nabi ofa ya maana.
Pamoja na yote hayo, Yanga ilisimama kidete chini ya Rais wao mpya, Hersi Said na kumbakisha kocha huyo raia wa Tunisia kwenye ardhi ya Tanzania kwa ajili ya misimu miwili zaidi.
Yanga haikufanikiwa kumbakisha tu kocha huyo bali pia kuepuka mtego waliojikwaa Simba wakati wakimruhusu kocha wao Sven Vandenbroeck akajiunge na FAR Rabat.
Rabat iliyaona mafanikio ya Sven akiwa Simba kwa mataji ya ligi na Kombe la FA alilowapa ikiwemo kuonyesha kiwango kizuri na ushindani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mwisho wakamng’oa Msimbazi.
Waarabu hao walitaka kurudia walichokifanya Simba mara ya mwisho na kisha kuwaachia Yanga jumba bovu la kutafuta kocha mpya mwenye maono na mfumo mpya, falsafa na itikadi tofauti na kuifanya timu hiyo ianze upya kwa kiasi fulani.
Nani anayejua pengine ndiyo ingekuwa mwanzo wa Yanga kuanza kutetereka. Tusijisahaulishe kuwa alipoondoka Sven Simba akaja Didier Gomez ambaye alijitahidi kufanya vyema lakini vyeti vikamuondoa, akatua Pablo Franco ambaye kila mmoja anajua nini kimetokea msimu uliomalizika hivi karibuni.
Yawezekana kishabiki Yanga wanafuraha yao juu ya mkataba mpya wa Nabi lakini kihesabu za soka Yanga wamefanya jambo limekuwa jepesi kwao hasa kwenye uti wa mgongo wa timu, benchi la ufundi.
Msimu ujao Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa na inahitaji kutikisa kama vile ilivyofanya Simba takriban misimu mitano iliyopita, hivyo kama wangekubali kufanya mabadiliko ya kocha ingewagharimu moja kwa moja kwenye michuano hiyo kulingana na mazingira halisi ya kikosi hicho.
Kukua kisoka si tu kujua kutumia pesa kwenye kusajili na kuingia mikataba na wadhamini bali hata kupiga hesabu ndogo zenye matokeo makubwa ni mabadiliko bora kwa Yanga kuelekea msimu ujao, wameamini ndani ya Nabi na bado wana imani naye kubwa, na pengine imani yao itawaponya!
Soka Nabi aongeza mkataba Yanga
Nabi aongeza mkataba Yanga
Read also