Na mwandishi wetu
Yanga SC imesaini mkataba mpya wa udhamini na Kampuni ya SportPesa wenye thamani ya Shilingi 12.3 bilioni ambao utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkataba wa awali wa SportPesa na Yanga uliodumu kwa miaka mitano umemalizika mwishoni mwa msimu uliopita na uongozi wa kampuni hiyo ya Michezo ya Kubashiri umeonesha kuvutiwa na Yanga katika kipindi kilichopita.
Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika leo jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli ya Johari Rotana ambapo imefafanuliwa kuwa kiasi hicho cha fedha kwa miaka mitatu mgawanyo ni Shilingi 4.1 bilioni kwa mwaka ikiwa ni tofauti na mkataba uliopita uliokuwa na thamani ya Sh 5.2 bilioni 5.2 kwa miaka mitano ambapo Yanga walikuwa wakichukua Sh bilioni moja kwa mwaka.
“Hii ni historia kwa klabu ya Yanga kwani kwenye mkataba wa awali, thamani ya mkataba kwa miaka yote mitano ilikuwa Sh. bilioni 5.2 yaani bilioni moja kwa mwaka lakini kwenye mkataba huu mpya Yanga itavuna zaidi ya Sh bilioni nne kwa mwaka,” alisema Mkurugenzi wa Utawala Sportpesa, Tarimba Abbas ambaye pia ni mbunge wa Kinondoni.
Tarimba ambaye pia amewahi kuwa Rais wa klabu hiyo miaka kadhaa nyuma ameeleza kuwa mbali ya mkataba huo mnono pia Yanga itapata bonasi ya Sh 150 milioni iwapo itatwaa taji la Ligi Kuu NBC na bonasi ya Sh 112 milioni kama itabeba taji la FA na Shilingi 75 milioni kama watatinga fainali ya michuano hiyo.
Tarimba ameeleza kuwa wakati wanaingia kwenye biashara ya ‘betting’ malengo yao makubwa ilikuwa ni kusaidia michezo na anafurahi kuona wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kwa kipindi cha miaka mitano nyuma wameweza kuweka utulivu kwa klabu kubwa za Simba na Yanga ambazo kabla ya hapo kidogo hali ya kifedha haikuwa nzuri sana.
Kwa upande wake rais mpya wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said ameipongeza Kampuni ya SportPesa kwa kufikia makubaliano hayo ambayo yameongeza thamani ya Yanga.
Hersi amesema watahakikisha wanatekeleza yaliyopo kwenye mkataba huo, na anaamini kwao itawaongezea ari ya kufanya vizuri na kutetea mataji yote ambayo wameyabeba msimu uliopita ikiwemo kwenye michuano ya kimataifa.
“Nashukuru sana Kampuni ya SportPesa kutokana na kuiongezea thamani klabu yetu, niwahakikishie kwamba udhamini huu umetupa deni la kuhakikisha msimu ujao tunafanya vizuri zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita na tutahakikisha hilo linatimia,” alisema Hersi.
Katika hafla hiyo Kampuni ya Sportpesa pia wameikabidhi klabu hiyo bonas ya Sh 100 milioni baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu uliopita wa 2021/22.
Soka Yanga yalamba bilioni 12 za SportPesa
Yanga yalamba bilioni 12 za SportPesa
Read also
