Milan, Italia
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Aaron Ramsey ameachana na klabu ya Juventus ya Italia baada ya mkataba wake kufutwa.
Ramsey ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya Wales alifikia hatua hiyo baada ya pande mbili kukaa na kukubaliana kuufuta mkataba wa mchezaji huyo ambaye alijiunga na Juventus mwaka 2019 akiwa mchezaji huru lakini aliitumikia timu hiyo hadi nusu ya msimu wa 2021/22 alipouzwa kwa mkopo katika klabu ya Rangers ya Scotland.
Msimu wa 2022/23 unaotarajia kuanza baadaye mwezi ujao ulitarajiwa kuwa wa mwisho kwa Ramsey na Juventus huku akiwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakilipwa Pauni 400,000 kwa wiki lakini sasa yuko huru kujiunga na timu yoyote kwani anatakiwa kujiimarisha kiuchezaji akiwania kuiwakilisha Wales kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar, Novemba mwaka huu.
Ramsey mwenye umri wa miaka 31 sasa, msimu wa 2021/22 haukuwa mzuri kwake kwani aliichezea Juventus katika mechi tano tu na kwa sasa tayari anahusishwa na mipango ya kurudi katika klabu yake ya zamani ya Cardiff City ingawa suala la mshahara wake linatarajia kuzua mjadala kabla ya kuamua kumsajili au kutomsajili sambamba na majanga ya kuwa majeruhi yaliyomuandama katika siku za karibuni nayo pia yanaweza kuwa kikwazo katika usajili wake.
Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri alimuondoka Ramsey katika ziara za maandalizi ya msimu wa 2022/23 nchini Marekani jambo ambalo linaonyesha kuwa hayumo kwenye hesabu za kocha huyo. Wengine walioondolewa kwenye msafara huo ni Marko Pjaca, Adrien Rabiot, Federico Chiesa, Arthur Melo, Mattia de Sciglio na Kaio Jorge.
Kimataifa Ramsey, Juventus waachana
Ramsey, Juventus waachana
Read also
