Manchester, England
Hatimaye mshambuliaji wa Manchester United, Cristiano Ronaldo ametua katika jiji la Manchester akitarajiwa kufanya mazungumzo na kocha Erik ten Haag, mazungumzo yatakayotoa hatma ya mchezaji huyo kama atabaki au ataachana na klabu hiyo.
Ronaldo alitarajiwa kuungana na wachezaji wenzake wa Man United Julai 4 mwaka huu kwa ziara ya maandalizi msimu wa 2022/23 katika nchi za Thailand na Australia lakini hakutokea kwa kilichoelezwa kuwa ni majukumu ya kifamilia huku ikidaiwa kwamba anataka kuihama timu hiyo.
Awali Ten Hag alisema kwamba alifanya mazungumzo na Ronaldo kabla ya ziara hiyo, mazungumzo ambayo alidai yalikuwa mazuri na yanabaki kuwa siri yao wawili ingawa uvumi kuhusu mchezaji huyo aliyebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake kutafuta maisha sehemu nyingine umezidi kupamba moto licha ya Ten Haag kusisitiza kwamba hauzwi.
Katika msimu uliopita, Ronaldo, mwenye umri wa miaka 37 alikuwa ndiye kinara wa mabao Man United kwa mabao yake 24 huku akishika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu England na timu yake ikimaliza ligi hiyo katika nafasi ya sita na hivyo kukosa nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa jambo ambalo inadaiwa ndilo linalomfanya Ronaldo atake kuondoka katika klabu hiyo itakayoshiriki Europa Ligi.
Chelsea na Bayern Munich zilizotajwa kumtaka zimetangaza kumtoa katika hesabu zao wakati Atletico Madrid ambayo Jumamosi hii itaumana na Man United nchini Norway katika mechi ya kirafiki ikionekana kumtaka licha ya baadhi ya mashabiki wake kupinga usajili huo.
Baada ya mechi na Atletico, siku inayofuata Man United itacheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Rayo Vallecano ikiwa nyumbani Old Trafford na baada ya hapo itajipanga kwa ajili ya kuanza mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England Agosti 7 dhidi ya Brighton.
Kimataifa Ronaldo, Ten Haag wateta
Ronaldo, Ten Haag wateta
Related posts
Read also