Na mwandishi wetu
Siku nne baada ya TFF kumfungia msemaji wa Yanga, Haji Manara kujihusisha na shughuli za soka kwa miaka miwili na kumtoza faini ya Sh 20 milioni, Manara ameibuka leo na kudai kwamba ataendelea kuwa msemaji wa Yanga hadi atakapopata nakala ya hukumu ya adhabu aliyopewa.
Julai 21, kamati ya maadili inayoongozwa na wakili Kichere Mwita ilitangaza adhabu hiyo kwa Manara akidaiwa kufanya kosa la kumvunjia heshima Rais wa TFF, Walace Karia Julai 2 tukio lililotokea kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Coastal Union.
Maneno ya kumshalilisha Karia ambayo Manara anadaiwa kuyatamka siku hiyo ni pamoja na kumwambia,”wewe unanifuatafuata sana na hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote nina uwezo wa kukufanya lolote na huna uwezo wa kunifanya lolote.”
Manara hata hivyo baadaye alijitokeza na kuomba radhi lakini kamati ya maadili haikukubaliana na maombi hayo, badala yake ikaamua kuendelea kusikiliza shauri hilo lililowasilishwa mbele yao na sekretarieti ya TFF kwa madai kuwa kuomba msamaha ni tendo la kawaida na haliwezi kufuta shauri lililokuwa mbele yao.
Akifafanua kuhusu mkasa wake na Karia leo na msamaha aliowahi kumuomba kiongozi huyo, Manara alisema kwamba ni Karia ndiye aliyeanza kumvunjia heshima mbele ya watu zaidi ya mara moja tangu akiwa Simba jambo ambalo amekuwa akilivumilia na aliamua kuomba msamaha kwa nia ya kujishusha ili hali itulie japo hakuwa na kosa lolote.
Akizungumzia kupinga adhabu aliyopewa, Manara alisema kwamba wameomba mara tatu nakala ya hukumu lakini wahusika hawakuwa tayari kuwapa kwa alichodai kuwa ni hofu ya wao kukata rufaa mara watakapopata hukumu hiyo.
Manara pia alisisitiza hoja ya awali iliyotolewa na mawakili wake kuhusu kanuni za TFF zilizotumika kumhukumu kuwa si halali kwa kuwa hazijasajiliwa na BMT hoja ambayo anasema kamati ya maadili iliitupa kwa madai kwamba kinachotakiwa kusajiliwa ni katiba na si kanuni.
Alielezwa kushangazwa na hatua ya kamati hiyo kupinga kanuni zilizowekwa na baraza la michezo ambalo lipo kisheria na hata ukienda kwenye ofisi za baraza wameandika kabisa kwamba kanuni zinatakiwa kusajiliwa lakini akawashangaa TFF kulikataa jambo hilo.
Akizungumzia ukubwa wa adhabu aliyopewa, Manara alisema kwamba yeye amekuwa binadamu wa kwanza Tanzania kupewa adhabu kubwa katika mpira. “Yaani mimi ndiye nimekuwa kama adui mkubwa kama Amrish Puri,” alisema akimtaja Amrish Puri, nyota wa filamu za Bollywood aliyesifika kwa kuigiza vizuri matukio ya kibabe na kikatili.
Manara aliongeza kwamba yote yanayoendelea dhidi yake kwa wakati huu, lengo ni kuhakikisha hashiriki wiki ya Mwananchi.
Soka Manara: Nitaendelea kuwa msemaji Yanga
Manara: Nitaendelea kuwa msemaji Yanga
Related posts
Read also