Na mwandishi wetu
Msemaji wa klabu ya soka ya Yanga, Haji Manara amefungiwa kutojihusisha na mambo ya soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili pamoja na kutozwa faini ya Sh 20 milioni.
Adhabu hiyo iliyotolewa leo na Kamati ya Maadili ya TFF inaanza rasmi leo, imekuja baada ya Manara kukutwa na hatia kwa makosa ya kumvunjia heshima Rais wa TFF, Wallace Karia.
Wiki takriban mbili zilizopita sekretarieti ya TFF ilifungua shauri kwenye kamati hiyo dhidi ya Manara baada ya kutokea sintofahamu kati ya Manara na Karia kwenye jukwaa kuu, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Coastal Union.
Katibu Mkuu wa kamati hiyo, Walter Lungu wakati akisoma hukumu hiyo alisema kwamba kamati ilianza kukutana tangu Julai 11, mwaka huu kwa ajili ya shauri hilo na ilisikiliza usahihidi wa pande zote mbili kabla ya kutoa humu hiyo.
Alisema kwamba sekretarieti ya TFF iliwasilisha kwao mashtaka ikionyesha kuwa siku ya tukio Manara alimshambulia Karia kwa kumwambia: “Wewe unanifuatafuata sana na hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote nina uwezo wa kukufanya lolote na huna uwezo wa kunifanya lolote.”
“Manara katika utetezi wake wa maandishi juu ya shauri hilo alisema yeye si kichaa kwa hiyo hawezi kutamka maneno hayo mbele ya watu bila ya kuwa amechokozwa na hakukuwa na kutukanana zaidi ya kutofautiana kidogo kati yake na ndugu Karia.
“Pia, mlalamikaji alisema kuwa maneno yake hayawezi kuchukuliwa kama vitisho au kumzuia Karia asitekeleze majukumu yake, itakuwa si haki kumshtaki kuwa amemkashifu Rais na wala maneno yake hayakuwa ya kuudhi.
“Kamati imejiridhisha pasipo na shaka kuwa Manara ametenda makosa hayo, kamati imemtia hatiani baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mlalamikaji na utetezi wa mlalamikiwa. Haji Manara anafungiwa kutojihusisha na shughuli za mchezo wa mpira wa miguu ndani ya nje ya nchi kwa miaka miwili na anatozwa faini ya Sh milioni 20, haki ya kukata rufaa kwa pande zote mbili iko wazi,” alisema Lungu. Muda mchache baada ya hukumu hiyo, Manara aliandika hivi kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram: “Iwe ni Jambo la kheri au shari, neno langu kuu ni kumshukuru muumba mbingu na ardhi kwa neno moja kubwa na lenye maana pana sana, Al-Hamdulillah. Asante mpira wa miguu.”
Manara aliwahi pia kufungiwa na shirikisho hilo, mwaka 2017 akiwa ofisa habari wa Simba. Kamati ya Nidhamu ya TFF ilimfungia kwa mwaka mmoja kutojihusisha na soka na kumtoza faini ya Sh milioni tisa baada ya kukutwa na hatia ya kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na kuingilia utendaji wa shirikisho hilo lakini miezi michache baadaye ilimsamehe na kumfungulia tena.
Manara pia bado ana kesi nyingine kwenye kamati hiyo akilalamikiwa na Simba kutoa shutuma zisizo za kweli dhidi ya klabu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.