Madrid, Hispania
Kukaa klabu moja miaka 10 si jambo dogo hasa klabu hiyo ikiwa ni Real Madrid, Luca Modric si tu amekaa klabu hiyo kwa miaka 10 bali ni miaka ya mafanikio, mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano, ni mafanikio yanayotosha kupigiwa saluti, hata mastaa walioimbwa miaka ya karibuni, Cristiano Ronaldo na Lionell Messi hawana rekodi ya kuchukua taji hilo kubwa mara tano katika klabu moja.
Messi kwa mfano amelitwaa taji hilo mara nne na Barcelona kama ilivyo kwa Ronaldo aliyelitwaa mara nne na Real Madrid na mara moja na klabu nyingine (Man United) hivyo kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya rekodi ya Modric inabaki kuwa ya kipekee katika klabu ya Real Madrid, amelibeba taji hilo kuanzia msimu wa 2013/14, 2015/16, 2016/17, 2017/18 na 2021/22.
Katika wakati wote huo, Modric ameonyesha uwezo wake kuwa ni mchezaji wa kiungo mwenye mbinu, kasi, uwezo wa kuusoma mchezo, kupiga chenga na kutoa pasi za uhakika na makini katika kudhibiti mashambulizi ya timu pinzani, sifa ambazo hapana shaka ndizo zinazomuwezesha kuendelea kuichezea Real Madrid licha ya umri wake kuwa mkubwa.
Sifa moja kubwa ya Real Madrid ni kusajili wachezaji mastaa wa bei mbaya na kuachana nao kiwango kinapoanza kushuka au wanapofikia miaka 30 na zaidi, imekuwa hivyo kwa kina Zinedine Zidane, Luis Figo, Ronaldo de Lima, Roberto Carlos, Raul Gonzalez, David Beckham na wengineo ambao hujikuta wakiondoka au kutoongezewa mikataba kama ilivyokuwa hivi karibuni kwa Gareth Bale na ilikuwa hivyo hata kwa Sergio Ramos na Cristiano Ronaldo, vipi mchezaji mwenye miaka 37?
Kwa Modric ni tofauti, tangu atue Real Madrid akiwa na miaka 27 ameendelea kuwapo na hadi sasa ana miaka 37 katika hali ambayo haikutarajiwa klabu imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja na hivyo kama ni kuondoka anatarajia kuondoka akiwa na miaka 38, si haba ni rekodi nzuri na haitoshangaza akiongezewa tena mwaka mmoja kwani bado anaonekana yuko vizuri.
Angekuwa kipa ingeonekana kawaida lakini kwa mchezaji wa ndani tena wa nafasi ya kiungo ni nadra jambo hilo kutokea hasa kwa klabu ya Real Madrid ambayo rais wake Florentino Perez na vigogo wenzake wamekuwa na sifa ya kuwa wagumu au kusita kumuongezea mkataba mchezaji ambaye umri wake unazidi miaka 30 (achana na 37) na kama ataongezewa basi ni mwaka mmoja au miwili.
Na ndio maana baada ya klabu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ulioisha hivi karibuni wa 2021/22 iliaminika kuwa Modric ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Croatia huo ungekuwa msimu wake wa mwisho lakini kocha Carlo Ancelotti alipoulizwa kuhusu hilo alisema, “Modric bado hajasaini mkataba lakini kimsingi ni kama vile ana mkataba wa maisha hapa.” kwa kauli hiyo haikushangaza kuona mchezaji huyo akiongezewa mkataba.
Wakati anatua Real Madrid mara ya kwanza mwaka 2012 akitokea Tottenham ilionekana kama klabu hiyo imesajili mchezaji ambaye hakuwa na hadhi ya kuichezea timu hiyo lakini mambo yakabadilika kila msimu na umuhimu wake kuzidi kuonekana na hatimaye amefikisha miaka 10 yenye mafanikio huku akiendelea kuhitajika.
Ukiachana na mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Modric pia ana tuzo ya Ballon D’ Or aliyoibeba mwaka 2018, ni tuzo iliyothamini mchango wake katika klabu ya Real Madrid ambayo ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huo pamoja na kuifikisha timu ya Taifa ya Croatia katika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Dunia.
Na hadi sasa kwenye timu ya Taifa ya Croatia, Modric anashika rekodi ya kuichezea timu hiyo mara nyingi akiwa tayari amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Darijo Srna aliyekuwa akishika nafasi ya kwanza kwa kuichezea timu hiyo mara nyingi, mara 134.
Kabla ya Real Madrid, safari ya Modric ilianzia kwao Croatia katika klabu ya Dinamo Zagreb ambayo ilimsajili akiwa na miaka 16, kabla ya hapo alionyesha kipaji na kupelekwa Hajduk Split, klabu maarufu na yenye utajiri katika mji wa Dalmatia lakini umbile dogo, kuonekana mwepesi na asiye na nguvu vilimkwaza kujiunga na timu hiyo hadi alipokwenda Italia na kuonyesha kipaji na uwezo wake katika mashindano ya vijana.
Mwaka 2003 aliuzwa kwa mkopo katika klabu ya Zrinjski ya Bosnia, akiwa na miaka 18 tu uwezo wake ulimfanya awe mwanasoka bora wa mwaka katika Ligi Kuu Bosnia na kauli yake kubwa ya wakati huo inayokumbukwa hadi leo ni pale aliposema, “mtu anayeweza kucheza soka kwenye Ligi Kuu Bosnia, huyo anaweza kucheza popote.” Na ndicho kilichojitokeza.
Alirudi Croatia mwaka 2004 na kujiunga na Inter Zapresic kwa msimu mmoja huku kipaji kikiendelea kujidhihirisha na mwaka huo huo alipewa tuzo maalum ya mwaka ya Croatian Football Hope of the Year kabla ya kurudi katika klabu yake ya awali ya Dinamo Zagreb ambayo baada ya kumuona ni lulu ikamsainisha mkataba wa miaka 10 katika msimu wa 2005/06.
Lulu ilijidhihirisha, mwaka 2008 ilibidi mwenyekiti wa Tottenham Daniel Levy asafiri mwenyewe kwa haraka hadi Zagreb ili kumpata Modric, hiyo ni baada ya kubaini kuwa Man City na Newcastle nao walikuwa wakimtaka mchezaji huyo lakini ni Levy aliyefanikiwa kumsajili kwa Pauni 16.5 milioni.
Kwa kipindi chote alichokuwa Tottenham, Modric aliendelea kuipa heshima na mafanikio klabu hiyo na kuwa moja ya klabu zinazowatetemesha vigogo wa Ligi Kuu England hadi Ulaya.
Katika msimu wa 2010/11, Modric alipewa na klabu ya Tottenham tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka lakini aliyekuwa kocha wa Man United, Sir Alex Ferguson alisema kwamba kwake yeye angemchagua Modrić kuwa mwanasoka bora wa msimu.
Kabla ya kutua Real Madrid Agosti 2012, Chelsea walikuwa wa kwanza kuonyesha nia ya kumtaka Modric lakini ofa yao ya Pauni 22 milioni ilikataliwa, wakaongeza hadi Pauni 27 milioni lakini bado Levy alikataa licha ya Modric mwenyewe kuonyesha nia ya kutaka kuondoka Tottenham na hatimaye ofa ya Real Madrid inayotajwa kufikia Pauni zaidi ya 28 milioni ikakubaliwa na Modric akaondoka.
Modric ni mume wa Vanja Bosnic ambaye walifunga ndoa Mei, 2010 baada ya kuwa wapenzi kwa miaka minne, ndoa yao iliandamana na hafla ndogo isiyo ya kifahari katika jiji la Zagreb na mwaka mmoja baadaye walifanya hafla nyingine kanisani, hadi sasa wana watoto watatu, mvulana Ivano (12) na wasichana Ema (8) na Sofia mwenye umri wa miaka minne.
Nje ya soka, Modric ambaye ni mkristo wa dhehebu la kikatoliki si mtu wa kujitokeza hadharani mara kwa mara, anapenda kufanya mambo yake chinichini, anazungumza vizuri kiingereza, kihispania na lugha ya kwao Croatia.
Kimataifa Saluti kwa mkongwe Luca Modric
Saluti kwa mkongwe Luca Modric
Related posts
Read also