Na mwandishi wetu
Hatimaye rasmi usiku wa kuamkia leo, Yanga imekata mzizi wa fitina kwa kumtambulisha kiungo wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki kama mchezaji wao mpya baada ya dili hilo kuvuma kwa muda mrefu huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda mpango wa kumsajili mchezaji huyo ungefeli.
Kwa kipindi cha wiki kadhaa mashabiki wa Simba na Yanga wamekuwa wakishambuliana kwa maneno ya utani hasa baada ya Yanga kuchelewa kumleta nchini mchezaji huyo licha ya kudai kwamba tayari wameshamsajili na hata kuonyesha picha zake jambo ambalo hata hivyo halikuwazuia mahasimu wao wa Simba kuwabeza mara kwa mara.
Ki ametua Yanga baada ya vigogo wa timu hiyo kufurahishwa na uwezo wake aliouonesha msimu uliopita akiwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast hasa baada ya kuifunga Simba mara mbili walipokutana kwenye michezo miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Kiungo huyo aliyekuwa akiwindwa na Simba pia, imeelezwa kuwa amepewa mkataba wa miaka miwili kwa ada ya usajili inayotajwa isiyopungua kitita cha Dola za Marekani 200,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 460.
Mchezaji huyo anayemudu vyema nafasi za kiungo mshambuliaji na pembeni pia amekuwa mhimili mkubwa kwa Asec ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ivory Coast maarufu Ligue 1.
Kwa msimu huo uliomalizika hivi karibuni, Ki amehusika kwenye utengenezaji wa nafasi za kufunga mabao takriban 39 na kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vyema katika nafasi hiyo na kuongezeka thamani kufikia zaidi ya Dola za Marekani 150,000.
Ujio wa Ki kwenye timu hiyo unaifanya Yanga kuwa na jumla ya wachezaji wapya watano ambao tayari imewatambulisha mpaka sasa kuelekea msimu ujao ikijipanga kuutetea ubingwa Ligi Kuu ya NBC Bara na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imetambulisha usajili wa wachezaji wa kigeni mpaka sasa, ukiachana na Ki wengine ni beki wa kushoto, Joyce Lomalisa kutoka GD Interclub ya Angola, kiungo wa kati, Gael Bigirimana aliyekuwa akikipiga Glentoran inayoshiriki Ligi Kuu ya Ireland.
Washambuliaji waliotua ni Lazarous Kambole kutoka Kaizer Chiefs na Bernard Morrison aliyemaliza mkataba wake Simba na kurejea Yanga ambayo aliwahi kuichezea kwa miezi sita kabla ya kwenda Simba na kudumu kwa miaka miwili.
Soka Aziz Ki akata mzizi wa fitina
Aziz Ki akata mzizi wa fitina
Related posts
Read also