Na mwandishi wetu
Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu 2021/22, George Mpole amekataa kufananishwa na washambuliaji wengine wa Tanzania waliovuma kwa msimu mmoja, akisema yeye ataonesha zaidi kipaji alichonacho kwa muda mrefu.
Mpole anayekipiga Geita Gold amefunga mabao 17 kwenye msimu uliomalizika hivi karibuni, akimpiku mpinzani wake wa karibu Fiston Mayele wa Yanga aliyefunga mabao 16.
Mpole alijinasibu kuwa kwenye soka kila mmoja ana ujuzi na malengo yake, hivyo yeye yuko tofauti na wengine katika hilo, akifafanua kuwa uwezo aliounesha hivi karibuni ni mwanzo na kwamba amepanga kuwa na mwendelezo mkubwa katika misimu inayofuata.
“Wapo waliopita lakini mimi ni Mpole, nadhani kila mtu yuko tofauti na kila mtu ana malengo yake, ukiangalia hata kwenye mahojiano yangu mengi nimeeleza namna ambavyo sijaegemea kucheza Tanzania sana.
“Nina ndoto zangu ambazo ni mwendelezo, kwa hiyo siwezi kusema kwamba msimu ujao nitaporomoka zaidi ya hapa, nimechukua tuzo ya ufungaji bora, huu ni mwanzo ni kama motisha kwenye ndoto zangu, kwa hiyo naweza kusema hapo bado sana,” alisema Mpole aliyewahi kuichezea Polisi Tanzania.
Mpole amekuwa lulu tangu kuanza kwa msimu wa 2021/22 akiiongoza timu hiyo iliyopanda daraja Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kumaliza kwenye nafasi ya nne huku akifunga mabao mawili kwenye mechi mbili alizoitwa kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars hivi karibuni.
Soka Mpole: Mimi si wa msimu mmoja
Mpole: Mimi si wa msimu mmoja
Related posts
Read also