Na mwandishi wetu Mtibwa Sugar kesho inatarajia kuikabili Tanzania Prisons kwenye mchezo wa pili wa mtoano kusaka tiketi ya kuendelea kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2022/23, ni mechi ambayo itaamua hatma ya Mtibwa kama ni kubaki katika ligi hiyo au la.
Mchezo huo ni wa pili baada ya ule wa awali uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Mtibwa kushinda kwa mabao 3-1 na sasa Mtibwa itakuwa nyumbani Uwanja wa Manungu, Morogoro kuendelea kuipigania nafasi hiyo na swali ni je Prisons wataisaidia Mtibwa kubali.
Kimsingi huo ni mchezo wa fainali kwa wawili hao kwani atakayeshindwa atalazimika kuingia kwenye kibarua kingine cha kupepetana na JKT Tanzania ya Championship ili kutetea nafasi yake na asishuke daraja.
Kocha Msaidizi wa Mtibwa, Awadh Juma alisema kwamba matokeo waliyoyapata awali, wameyafuta na wanajipanga huku wakiendelea kuwaheshimu wapinzani wao ili kulinda ushindi wao na pengine kufanya vizuri zaidi wakati Prisons nao wakitambua kwamba wana kazi ngumu ya kupindua matokeo.
“Yale ni matokeo ya mechi iliyopita ambayo imeshakwisha na hii ni mechi nyingine, tunahitaji kuongeza umakini zaidi, michezo ya mtoano inahitaji kuchezwa kwa mtego, kujipanga vizuri kwenye uwanja wa nyumbani kuendelea pale tulipoishia ili tutimize malengo,” alisema Awadh ambaye pia mchezaji wa zamani wa Simba SC.
Kocha msaidizi wa Prisons, Shaban Mtupa alisema watarekebisha makosa yao, wataingia na mbinu tofauti zaidi kuwasaidia kupata ushindi katika dakika 90 hizo za mwisho zilizoshikilia hatma yao.
“Tunajipanga kwa mchezo huu, mwanzoni walituzidi kwa mbinu na mchezo huu wa pili tutahakikisha tunapambana kwa uwezo wetu na kuwajenga wachezaji kisaikolojia kucheza kwa utulivu, nina imani tutafanya vizuri,”alisema.
Katika mechi hiyo, Mtibwa inahitaji sare yoyote au ushindi kwa ajili ya kujihakikishia nafasi ya kuendelea kucheza Ligi Kuu wakati Prisons wana kazi kubwa kwani watahitaji ushindi wa kuanzia mabao matatu na kuendelea huku pia wakizilinda nyavu zao zisiharibu uwiano wa mabao.
Msimu uliopita Mtibwa iliangukia tena kwenye michezo ya mtoano, ilicheza na timu ya Championship ya Transit Camp na kupata matokeo ya ushindi wa jumla wa mabao 4-2 na kubaki Ligi Kuu.
Soka Prisons kuibakisha Mtibwa Ligi Kuu?
Prisons kuibakisha Mtibwa Ligi Kuu?
Related posts
Read also