Na mwandishi wetu
Klabu ya Azam imeonesha kukamia safari hii kuelekea msimu ujao baada ya kutangaza usajili wa mchezaji Abdu Selemani ‘Sopu’ anayetajwa kila kona kwa sasa kutokana na umahiri aliounesha msimu uliopita wa 2021/22 akiwa na Coastal Union ya Tanga.
Huu ni mwendelezo wa Matajiri hao kutambulisha wachezaji wao wapya tangu wiki iliyopita na sasa Sopu anaingia kwenye orodha hii kwa usajili unaotajwa kuwagharimu Azam takriban Sh milioni 150.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito ameeleza kuwa mshambuliaji huyo amesajiliwa Azam baada ya makubaliano ya Coastal pekee kupewa Sh milioni 100 ya kuvunja kandarasi ya Sopu ya miaka miwili alioingia nao hivi karibuni.
“Nizungumzie kwa upande wetu, sisi kama Coastal baada ya makubaliano kulingana na mazungumzo yalivyokuwa juu ya Sopu, tukapewa Sh milioni 100 na pia nafikiri kutakuwa na makubaliano juu ya mchezaji mwenyewe na hiyo ni kwa upande wake,” alisema Tito.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kuwa awali dakika za mwisho kabla ya kukubaliana kwa dili hilo, maelewano yalikuwa kitolewe kiasi kisichopungua Sh milioni 150 kwa ajili ya hesabu ya jumla ya kumalizana na timu na mchezaji huyo ambaye pia alikuwa anatajwatajwa kuwaniwa na vigogo Simba na Yanga.
Sopu ambaye amewahi kupita kwenye kikosi cha timu ya vijana cha Simba B, amewashawishi Azam kwa kiwango cha hali ya juu alichokionesha msimu 2021/22 pamoja na kufunga mabao saba kwenye Ligi Kuu ya NBC na kutwaa kiatu cha ufungaji bora kwenye michuano ya Kombe la Azam (ASFC) kwa kufunga mabao tisa.
Mchezaji huyo anayemudu vema majukumu ya mshambuliaji wa pembeni na kati, pia aliibuka mchezaji bora wa fainali ya Kombe la Azam baada ya kufunga mabao matatu walipopoteza fainali hiyo dhidi ya Yanga kwa matuta 4-1 baada ya sare ya 3-3 kwenye dakika 120. Hat-trick ya kwenye fainali hiyo ilikuwa ya pili kwake kwenye michuano hiyo.
Usajili huo unakuwa usajili wa pili kwa Azam kwa wachezaji wa ndani baada ya Cleophas Mkandala aliyetokea Dodoma Jiji. Wengine ni Waivorycoast, Kipre Junior na Tape Edinho pia kiungo mkabaji wa Nigeria, Isah Ndala huku ikiwa tayari imewapa rasmi mkono wa kwaheri kipa Mathias Kigonya raia wa Uganda na kiungo mzawa, Frank Domayo.
Soka Sopu wa Coastal atua Azam
Sopu wa Coastal atua Azam
Related posts
Read also