Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga kimeongezewa nguvu kuelekea mchezo wake wa leo baadaye wa fainali ya Kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Union baada ya mfadhili wa timu hiyo, Ghalib Said Mohamed (GSM) kutua jijini Arusha au A Town kuushuhudia mchezo huo.
Yanga inatarajia kuivaa Coastal majira ya saa 9.00 alasiri kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ikitazamia kutwaa ndoo yao ya pili msimu huu baada ya siku chache nyuma kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara 2021/22 bila ya kupoteza mchezo kwenye mechi 30 za ligi.
Imeelezwa kuwa GSM ametua jijini Arusha alfajiri ya kuamkia leo, tayari kwa ajili ya kuushuhudia mtanange huo unaosubiriwa kwa hamu licha ya Coastal kupoteza mechi zote mbili walizokutana na Yanga kwenye ligi msimu huu.
Shangwe za mashabiki na wadau wa Yanga zimefumuka jijini humo baada ya taarifa za kuwasili kwa ‘mnene’ huyo ambaye amehusika kwa kiwango kikubwa kuirejesha Yanga kwenye mstari wake baada ya kuyumba kwa takriban misimu minne iliyopita.
Hata hivyo, hii ni mara ya pili kwa GSM kuishuhudia Yanga ikicheza fainali. Mara ya mwisho aliishuhudia timu hiyo ikiwachapa Simba kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya suluhu ya dakika 90 kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Soka Mfadhili Yanga atua A Town
Mfadhili Yanga atua A Town
Related posts
Read also