Na mwandishi wetu
Fiston Mayele ni kama vile amekuwa mpole baada ya George Mpole kumaliza Ligi Kuu ya NBC akiwa kinara wa mabao kwa kufunga jumla ya mabao 17 wakati Mayele amemaliza akiwa na mabao 16, ni kama vile ameshindwa kutetema na kujikuta akitetemeshwa na Mpole.
Kwa kipindi kirefu mbio za kusaka tuzo ya mfungaji bora wa ligi hiyo ilikuwa kati ya washambuliaji watatu, Mayele wa Yanga, Mpole wa Geita Gold na Reliants Lusajo wa Namungo, watatu hao mmoja wao alikuwa anaelekea kutwaa tuzo hiyo.
Baadaye, pumzi ya Lusajo ikakata wakati akiwa na mabao 10 na kuwaacha Mpole na Mayele wakifukuzana katika ushindani ambao ulikuwa wa mabao mawili na wakati mwingine bao moja.
Mayele kwa kipindi kirefu alikuwa ndiye kinara, akifumania nyavu mara kwa mara huku akinogesha mabao yake kwa staili ya kutetema ambayo pia imekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini, hakuna ubishi kwamba imani waliyokuwa nayo mashabiki wengi hasa wa Yanga ni kwamba tuzo hiyo hatimaye ingeangukia kwa mshambuliaji huyo kutoka DR Congo.
Zikiwa zimebaki kama mechi tano hivi za ligi, mitetemo ya Mayele ikaanza kupungua huku Mpole naye akionekana kutishia tuzo iliyoaminika kuwa ya Mayele, tofauti ya wawili hao ikawa ni mabao mawili au moja, ikawa Mayele akitetema Mpole anatupia.
Hatimaye Mpole naye akapata nafasi ya kukaa juu na kumshusha Mayele katika nafasi ya pili, hali ikaendelea kuwa hivyo kwa kipindi kirefu, Mayele akiwa juu wiki hii, wiki inayokuja Mpole anatupia na kushika usukani hadi walipofungana wote wakiwa na mabao 16.
Mechi za mwisho za ligi zilizopigwa jana mashabiki wakawa wanasubiri kwa hamu ili kujua nani atabeba tuzo ya mfungaji bora, wakati Yanga ikiumana na Mtibwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Geita ilikuwa ugenini dhidi ya Coastal Union, katika mechi hizo Mpole akafunga bao lililoifanya timu yake kuambulia sare ya bao 1-1 wakati Yanga nayo ikaichapa Mtibwa bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Dennis Nkane.
Kuna kila sababu ya kumpongeza Mpole kwa mafanikio aliyofikia kwani ameshinda tuzo ya ufungaji bora katika ligi ambayo imeanza kuwa ngumu, ligi iliyosheheni washambuliaji kutoka nje ya nchi, hapo unawazungumzia kina Chris Mugalu, Meddie Kagere wa Simba, bila kumsahau John Bocco, washambuliaji ambao msimu huu nao walitarajiwa kung’ara lakini pengine ugumu wa ligi umewakwaza.
Katika orodha hiyo ya washambuliaji mahiri mwingine ni mshindani mkuu wa Mpole, Mayele ambaye vita yao sote tuliishuhudia jinsi ilivyokuwa ngumu lakini Mpole amefanikiwa kutoboa.
Pia mwingine wa kupongezwa ni Mayele ambaye amesababisha kuwapo ushindani mkubwa katika mbio za kusaka tuzo ya mfungaji bora huku akionyesha uwezo na kufunga mabao ambayo yaliipendezesha ligi, kwa haraka haraka unaweza kulitolea mfano bao lake katika mechi dhidi ya Azam, alipounganisha mpira wa juu uliompita beki Aggrey Morris, mashabiki wa Yanga wanaliita bao lile kuwa ni la kideoni.
Zaidi ya yote mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona nini atakifanya Mpole katika ligi ya msimu ujao, kwani si mbali, imekabaki takriban mwezi mmoja na wiki kadhaa kabla ya kuanza kwa ligi hiyo ya msimu wa 2022/23, je Mpole atauendeleza moto wake kama ilivyokuwa msimu wa 2021/22 au ni mshindani wa msimu mmoja tu? .
Katika mechi nyingine za mwisho za ligi zilizopigwa jana matokeo ni kama ifuatavyo…
Kagera Sugar 0-0 Polisi Tanzania
Dodoma Jiji 1-0 KMC
Ruvu Shooting 1-0 Prisons
Mbeya City 1-1 Namungo
Mbeya Kwanza 0-0 Simba
Azam 4-1 Biashara
Soka Mayele awa mpole kwa Mpole
Mayele awa mpole kwa Mpole
Related posts
Read also