Na mwandishi wetu
Wapinzani wa Yanga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA, Coastal Union wamefika alfajiri ya leo jijini Arusha au A Town kujiandaa mapema kwa ajili ya fainali hiyo itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Amri Abeid.
Coastal yenye maskani yake Tanga imekuwa ya kwanza kufika jijini humo wakati Yanga ikitarajiwa kuondoka Dar es Salaam jioni ya leo na kuwasili Arusha majira ya usiku.
Kocha Mkuu wa Coastal, Juma Mgunda amesema kuwa katika siku mbili hizi zilizobaki, watatoa maelekezo na kufanya mazoezi madogo madogo kwani maandalizi mengine ya nguvu kuelekea mechi hiyo walishafanya tangu kwao Tanga.
“Tumeshafika Arusha, na sasa kilichopo ni kuendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya mechi na itakuwa maelekezo na mazoezi madogo madogo ya kumalizia tu japo tunafahamu kuwa mchezo lazima uwe mgumu, ni fainali hii.
“Tumekutana na Yanga kwenye ligi msimu huu lakini hii ni mechi nyingine ya fainali, ni ya mtoano siyo ya ligi kwa hiyo ni mechi nyingine yenye mrengo mwingine kwamba hatuhitaji pointi, cha muhimu ni ushindi na hilo tumejiandaa nalo,” alisema Mgunda.
Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara alisema: “Tutaondoka saa 12 jioni (leo) kuelekea Arusha kwa ajili ya fainali ya Kombe la FA. Tunafahamu Coastal ni rafiki zetu, ndugu zetu tunawapenda lakini bado mwaka huu tuna jambo letu.
“Tunajua ubora wao ingawa kwenye ligi msimu huu wametupa pointi sita na bado hicho si kigezo, lazima tuutafute ushindi. Tutacheza fainali hiyo tukiwa hatutaki kuharibu furaha za Wananchi, tunataka kurejea na kombe jingine.”
Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu, wamekutana na Coastal mara mbili. Mechi ya kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na ya pili mabao 3-0 hivyo hii ni mechi nyingine kwa Coastal kujiuliza juu ya uwezo wake dhidi ya Yanga msimu huu na kuvuta hisia za wengi kuelekea mchezo huo.
Coastal imepenya hatua hiyo baada ya kuibamiza Kagera Sugar kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1 baada ya kumalizika dakika 90 za kawaida kisha ikaibonda Azam kwa penalti 6-5 baada ya kushindwa kufungana kwenye dakika 90.
Upande wa Yanga yenyewe ilitinga nusu fainali baada ya kuichapa Geita Gold kwa penalti 7-6 baada ya sare ya 1-1 katika muda wa kawaida wa mechi kabla ya kuitandika Simba bao 1-0 kwenye nusu fainali ya michuano hiyo.
Soka Coastal yatua A Town
Coastal yatua A Town
Related posts
Read also