Cardif, Wales
Winga wa zamani wa Man United, Ryan Giggs ameng’atuka rasmi katika nafasi ya kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Wales inayojiandaa na fainali za Kombe la Dunia na nafasi yake sasa inashikiliwa na aliyekuwa msaidizi wake, Robert Page.
Giggs ambaye amechukua uamuzi huo kutokana na tuhuma zinazomkabili za kumdhalilisha mpenzi wake wa zamani, Kate Greville, katika taarifa yake alisema: “Baada ya kufikiria kwa kina, nang’atuka katika nafasi yangu ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanaume ya Wales mara moja.”
“Imekuwa ni heshima na jambo lenye hadhi kwangu kuwa kocha wa nchi yangu lakini naona ni jambo sahihi kwa viongozi wa FA Wales, benchi la ufundi na wachezaji kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia bila kuwapo minong’ono na uvumi kuhusu kocha wao mkuu.
Mara baada ya taarifa hiyo ya Giggs, viongozi wa Chama cha Soka Wales (FAW) nao wakatoa taarifa yao wakimshukuru kwa kipindi alichokuwa akiinoa timu hiyo na wameridhika na uamuzi aliouchukua walioutaja kuwa ni kwa manufaa ya soka la Wales na kwamba mtazamo wao kwa sasa pamoja na timu ya Taifa upo kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar.
Kuondoka kwa Giggs kulitabiriwa na baadhi ya watu kutokana na kashfa iliyokuwa ikimuandama hasa baada ya awali kujipa likizo ingawa wapo ambao waliamini angeendelea kuwa na timu hiyo ambayo imefuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 64.
Giggs hata hivyo amekana kuwahi kumfanyia shambulio la mwili na aina yoyote ya udhalilishaji Kate licha ya kudaiwa mahakamani kwamba alimfanyia unyama huo Kate pamoja na dada yake aitwaye Gema Greville, matukio ambayo imeelezwa aliyatenda kati ya Agosti 2017 na Novemba 2020 wakati mwingine akiwa nyumbani kwake mjini Manchester.
Awali Giggs alilazimika kujipa likizo Novemba 2020 baada ya kukamatwa akihusishwa na kashfa hiyo lakini sasa ameamua kujiondoa moja kwa moja kwa alichodai kwamba hataki kwa namna yoyote maandalizi ya nchi yake kwenye fainali za Kombe la Dunia yaathiriwe au kuvurugwa na kesi inayomkabili na kama ni kurudi kuinoa timu hiyo atakuwa tayari kufanya hiyo hapo baadaye.
Giggs aliteuliwa kuinoa Wales Januari 2018 ambapo Page ambaye ni nahodha wa zamani wa Wales, amekuwa msaidizi wake tangu Agosti 2019.
Kimataifa Giggs ang’atuka Wales
Giggs ang’atuka Wales
Related posts
Read also