Na mwandishi wetu
Kiungo wa timu ya Coastal Union, Victor Akpan ameweka wazi kuwa itajulikana kama anaenda Simba au la baada ya kumalizana na Yanga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA utakaopigwa Julai 2, mwaka huu.
Akpan amekuwa akihusishwa kujiunga na Simba kwenye usajili huu wa dirisha kubwa kuelekea msimu ujao wa 2022-23 kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha akiwa na Coastal akiisaidia timu hiyo kutinga fainali ya Kombe la FA.
Mchezaji huyo raia wa Nigeria ameeleza kwamba anahisi kwa sasa ni muda sahihi zaidi kujikita kimaandalizi kwenye mechi mbili za Ligi Kuu ya NBC zilizobaki pamoja na ile ya fainali ya FA kisha akishamaliza majukumu hayo atakuwa kwenye wakati mzuri wa kufahamu hatma yake.
“Niseme sasa hivi nataka kuwa makini zaidi na michezo miwili ya ligi na fainali ya Kombe la FA, nahisi baada ya hapo nitajua kama naenda au siendi lakini Simba ni timu kubwa pamoja ya kwamba imekuwa na msimu mbaya, ni ndoto ya kila mtu kucheza pale, kwa hiyo kama nafasi inakuja kila mmoja angefurahia hilo,” alisema Akpan.
Pamoja na hayo lakini kumekuwa na taarifa kutoka duru mbalimbali kuwa mchezaji huyo ameshamalizana na Wekundu hao kwa kandarasi ya miaka miwili na kinachosubiriwa ni wakati sahihi wa kuweka wazi suala hilo.
Soka Akpan: Mambo ya Simba baadaye
Akpan: Mambo ya Simba baadaye
Related posts
Read also