Na mwandishi wetu
Zikiwa zimepita siku tatu tangu Yanga inyakue taji la Ligi Kuu ya NBC msimu huu, uongozi wa timu hiyo umetangaza utakuwa na mapumziko ya siku 15 tu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu ujao.
Pamoja na hayo, Yanga pia imeeleza mipango yake ya kuweka kambi nje ya nchi kwa takriban wiki tatu kabla ya kurejea nchini kujiandaa na mechi za awali za Klabu Bingwa Afrika na Ligi Kuu kwa ujumla.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Hersi Said amefafanua kwamba mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Juni 29 na fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Julai 2, watakuwa na siku chache za kurejea kwa msimu mpya hivyo ndiyo maana wamekuwa na siku chache za kupumzika.
“Mwisho wa msimu ni tarehe 29 lakini kuna mechi ya Julai 2 (dhidi ya Coastal Union), lakini ukiangalia haraka haraka tarehe 12 mpaka 14 Agosti, itakuwa mechi za kwanza za mzunguko wa kwanza wa Klabu Bingwa kwa hiyo ukiangalia kuna wiki nne mpaka tano tu za kuanza msimu mpya baada ya huu kumalizika.
“Kwa mazingira hayo sasa na wachezaji kwa kuwa wanahitaji kupumzika, kwa hiyo tutakuwa na mapumziko ya siku kama 10 au 15, na kwenye Julai 15 wachezaji wanatakiwa wawe tayari wameripoti kwa ajili ya kwenda ‘pre-season’.
“Tutakuwa na ‘pre-season’ ya wiki tatu nje ya nchi, baada ya hapo tutarudi kwa ajili ya Wiki ya Mwananchi, nadhani itakuwa Agosti 6. Na baada ya hapo wiki ijayo tutakuwa na mechi ya kwanza ya Klabu Bingwa na inaweza kuwa nyumbani au ugenini, kwa hiyo unaona muda ni mdogo,” alisema Hersi.
Yanga ambayo haijapoteza mechi mpaka sasa tangu kuanza kwa msimu, ilitawazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi baada ya kuifumua Coastal Union mabao 3-0 na kufikisha pointi 67 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine huku ikiwa imesaliwa na michezo mitatu mkononi.
Soka Yanga mapumziko siku 15 tu
Yanga mapumziko siku 15 tu
Related posts
Read also