Na mwandishi wetu
Yanga usiku wa leo imetawazwa rasmi kuwa vinara wa Ligi Kuu ya NBC Bara msimu wa 2021/22 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union.
Kwa ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga imefikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote na inakuwa imebeba taji ikiwa na mechi tatu kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
Alikuwa ni Fiston Mayele aliyeipatia Yanga bao la kwanza katika dakika ya 34 baada ya mabeki wa Coastal kuchelewa kuokoa mpira ambao ulikuwa katika eneo lao na ndipo Mayele alipouwahi na kupiga shuti la chinichini lililogonga mwamba na kujaa wavuni huku mlinda mlango wa Coastal, Mohamed Hussein akijaribu kurukia mpira huo ambao ulimshinda.
Yanga iliandika bao la pili dakika saba baada ya kuanza kipindi cha pili, bao lililofungwa kwa kichwa na Chiko Ushindi ambaye aliitumia vizuri krosi ya Mayele iliyotokea upande wa kulia ambapo Mayele alipiga krosi hiyo kwa staili ya kuukata mpira na mfungaji kuruka kwa staili ya kuchupa.
Coastal walionekana kuvurugwa na bao hilo lakini Mayele aliwavuruga zaidi kwa kuandika bao la tatu katika dakika ya 69 safari hii akiunganishiwa pande na Feisal Salum au Toto.
Coastal waliianza mechi hiyo vizuri na kuonyesha dalili zote za kutotaka kuwa daraja kwa Yanga kubeba taji mbele yao, walifanikiwa kuonyesha uwezo dakika 25 za mwanzo na kuwafanya Yanga wasiwe na madhara hali iliyotoa dalili za mechi hiyo kuwa ngumu kabla mambo hayajabadilika.
Kwa ushindi huo, Yanga inakuwa imebeba taji ambalo imelikosa kwa misimu minne ambayo hasimu wake Simba amekuwa akilibeba mfululizo huku mshambuliaji wao Mayele akifikisha mabao 16 katika ligi hiyo na hivyo kumpita George Mpole wa Geita Gold mwenye mabao 15 ambaye kwa muda mrefu wamekuwa wakichuana katika kuwania tuzo ya mfungaji bora.
Soka Yanga baba lao 2022
Yanga baba lao 2022
Related posts
Read also