Na mwandishi wetu
Ni kama vile Simba inataka kutibua furaha za ushindi wa ubingwa wa Yanga na kuwapooza mashabiki wao baada ya kutambulisha usajili wao mpya wa mshambuliaji hatari wa Zambia, Moses Phiri.
Hiyo ni kutokana na muda mchache uliopita, klabu hiyo kuweka wazi juu ya usajili huo wakati Yanga ikiwa dimbani ikipepetana na Coastal Union, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ikumbukwe Yanga pia ilikuwa ikitajwa kuvizia saini ya mchezaji huyo aliyekuwa anakipiga Zanaco kabla ya baadaye kubaini kuwa ameshamalizana na Simba na ni suala la muda kabla ya kutangazwa na Wekundu hao.
Leo (Jumatano) ilikuwa mechi muhimu kwa Yanga ambayo wameshinda mabao 3-0 na kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya NBC baada ya miaka minne kwa kufikisha pointi 67, pointi ambazo hazitafikiwa na timu nyingine kimahesabu kulingana na pointi za wanaomfuatia kwenye msimamo.
Simba imeeleza kumpa kandarasi ya miaka miwili mchezaji huyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii baada ya mchezaji huyo mwezi huu kumaliza kandarasi yake ya miaka miwili pia ndani ya Zanaco.
Msimu huu, Phiri ambaye makabrasha yake yanaonesha ana miaka 29 amefanikiwa kuifungia Zanaco mabao 14. Ndani ya miaka miwili ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 31.
Ujio wa Phiri ni kwa ajili ya kuziba pengo la Bernard Morrison ambaye amepewa mkono wa kwaheri Simba, miongoni mwa sababu zikihusishwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Baada ya Simba kulimaliza suala la Phiri inaelezwa kuwa sasa wamebakisha kunasa saini ya straika Cesar Manzoki raia wa DR Congo anayekipiga Vipers ya Uganda. Mwingine ni George Mpole wa Geita Gold anayeshikilia nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji msimu huu akiwa na mabao 15 na asisti tatu.
Hao wanatajwa kuja kuwa miongoni mwa warithi wa nafasi za Chris Mugalu na Meddie Kagere ambao zipo habari kuwa huenda wakapewa mkono wa kwaheri baada ya kumaliza mikataba yao.
Pia, Simba inatajwa kuwa kwenye mawindo makali ya kumnasa kiungo wa kati mwenye uwezo wa kucheza kiungo cha juu na chini pia, Morlaye Sylla wa timu ya taifa ya Guinea anayekipiga klabu ya Horoya ya Ghana.
Soka Moses Phiri rasmi Simba
Moses Phiri rasmi Simba
Related posts
Read also