Na mwandishi wetu
Taifa Stars leo imeshindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kufungwa mabao 2-0 na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2023.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Algeria waliandika bao lao la kwanza katika dakika mbili za nyongeza kabla ya timu hizo kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Rami Bensebaini.
Bao hilo lilitokana na mpira mrefu uliopigwa na Youcef Belail ambao ulikuwa unatoka nje lakini mchezaji mmoja wa Algeria akaurudisha ndipo mfungaji alipowazidi ujanja mabeki wa Stars kwa kuuwahi mpira wa juu na kuujaza wavuni kwa kichwa.
Stars inayonolea na kocha Kim Poulsen kutoka Denmark ilipambana na kuonyesha uhai ikitaka kurudisha bao hilo huku ikiwa makini katika kuzuia lakini mambo yaliharibika katika dakika ya 86 baada ya Mohammed Amoura kuipatia Algeria bao la pili. Amoura alifunga bao hilo baada ya kukimbia na mpira na kuwatoka mabeki wa Stars kabla ya kufumua shuti ambalo liligonga mwamba na kumrudia mchezaji mwenzake wa Algeria ambaye alimrudishia mfungaji ambaye aliukokota kabla ya kufumua shuti la juu lililojaa wavuni.
Stars katika mechi ya leo licha ya kipigo hicho lakini ilionyesha uhai na kulisakama mara kadhaa lango la Algeria lakini bahati haikuwa yao, mfano dakika ya 31,.Simon Msuva alimzidi ujanja beki wa Algeria na kupiga krosi ya chinichini ambayo Mbwana Samatta aliruka na kuupiga kichwa mpira huo ambao hata hivyo ulitoka nje.
Dakika tatu baadaye, Fei Toto alifumua shuti baada ya kuinasa pasi ya Samatta na kama si umahiri wa kipa wa Algeria, Stars ingeandika bao la kwanza.
Kwa ushindi huo, Algeria imeendelea kujiimarisha kileleni katika Kundi F ikiwa na pointi sita baada ya kuifunga Uganda mabao 2-0 katika mechi yake ya kwanza, Niger ni ya pili ikiwa na pointi mbili baada ya sare na Stars katika mechi yake ya kwanza na leo imepata sare nyingine pia ya bao 1-1 mbele ya Uganda Cranes. Stars na Uganda zote zina sare moja na zimepoteza mechi moja.
Katika mechi nyingine ya kufuzu Afcon 2023 iliyochezwa leo, Congo iliutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuilaza Gambia bao 1-0.
Kimataifa Stars yakwama kwa Mkapa
Stars yakwama kwa Mkapa
Related posts
Read also