Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imetangaza kuwa inategemea kumpata kocha mpya wa timu hiyo baada ya kukamilika mchakato wa mchujo na mazungumzo utakaodumu kwa takriban wiki mbili.
Mbali na hilo imeelezwa kuwa hadi sasa ni takriban makocha 100 wametuma wasifu wao kwa uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kurithi mikoba ya Pablo Franco aliyeondolewa kwenye kikosi hicho wiki moja iliyopita.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa mchakato huo umekuwa na wasifu wa makocha wengi kutoka Ulaya, Amerika ya Kusini na kocha mmoja kutoka Afrika ambaye hakutaja maelezo yake kwa kina.
“Kuhusu kocha tulipokea ‘CV’ takriban 100, kwa hiyo sasa kamati itakaa kupitia na kisha itachuja mpaka kufikia makocha 40. Baada ya hapo kamati itakaa tena wiki hii na kupitia kupunguza idadi hiyo mpaka watakapopatikana wanaotakiwa na kufanyiwa mahojiano.
“Mahojiano yanatarajia zaidi kuwa ya ‘online’ na kisha atakayepita atawekwa wazi. Kwa hapa Afrika kulikuwa na wasifu wa kocha mmoja aliyeomba, wengi wametoka Ulaya na Amerika ya Kusini,” alisema Ally.
Simba ilimuondoa Pablo na timu hiyo sasa ipo chini ya kocha msaidizi, Selemani Matola mpaka mwisho wa msimu huu.
Pablo alitimuliwa sanjari na kocha wa viungo, Daniel Castro kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo, ikishindwa kufikia malengo ya msimu kufuatia kupoteza makombe yote mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam, huku ikifeli kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiishia robo fainali.
Soka Mchujo mrithi wa Pablo waanza Simba
Mchujo mrithi wa Pablo waanza Simba
Related posts
Read also