Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya klabu ya soka ya Yanga, Malango Mchungahela, leo jijini Dar es Salaam ametangaza mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Julai 10 mwaka huu.
Mchungahela alitaja nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo kuwa ni rais, makamu wa rais na wajumbe wa mkutano mkuu ambapo katika nafasi ya rais na makamu, mwanachama atakayetaka nafasi hizo atatakiwa kulipia Sh 200,000 ambazo ni gharama ya fomu wakati kwa mgombea wa nafasi ya ujumbe fomu gharama yake ni Sh 100,000.
Mchungahela pia alitumia nafasi hiyo kutangaza muda wa wiki mbili zaidi kwa viongozi wa ngazi ya matawi kuhakikisha wanakamilisha chaguzi katika matawi yao kabla ya muda huo badala ya ule uliowekwa awali wa Mei 30.
Wanachama wenye nia ya kugombea nafasi hiyo watatakiwa kuchukua fomu na kurudisha, zoezi ambalo litafanyika kati ya Juni 5 hadi 9 wakati Juni 10 na 11 utafanyika mchujo baada ya wagombea kuitwa kwa barua na orodha ya awali ya wagombea baada ya mchujo itatoka Juni 12 wakati Juni 13 hadi 15 wenye pingamizi watatakiwa kuwasilisha.
Juni 16 hadi 18 pingamizi zote zitapitiwa na Juni 19 orodha ya awali itatangazwa na fursa ya kukata rufaa kwenye kamati ya rufani ya uchaguzi ya TFF itakuwa ni kati ya Juni 24 hadi 26 na baada ya hapo rufaa hizo zitasikilizwa kati ya Juni 27 hadi Julai mosi.
Kuanzia Julai 5 hadi 9 wagombea watapata nafasi ya kufanya kampeni kabla ya kuingia kwenye uchaguzi Julai 10.
Soka Uchaguzi Yanga Julai 10
Uchaguzi Yanga Julai 10
Related posts
Read also