Na Jonathan Haule
Uamuzi wa Yanga kuachana na Saido Ntibazonkinza umeacha maswali juu ya sababu ya mchezaji huyo kuachwa. Je ni utovu wa nidhamu au kiwango chake, na vipi mambo yake ya baadaye?
Katika taarifa ya Yanga iliyopatikana Jumatatu iliyopita, uongozi wa klabu hiyo umemshukuru mchezaji huyo kwa kuitumikia klabu yao kwa kipindi cha miaka miwili na kumuaga baada ya kumaliza mkataba wake Mei 30, 2022.
Je ni kwa nini hasa Yanga imefikia uamuzi huo, imechoka na huduma ya mchezaji huyo kwamba haimhitaji tena kwa kuwa kiwango kimeshuka na tayari kuna mchezaji wa kuziba nafasi yake au tatizo ni utovu wa nidhamu?
Kabla ya kuagwa rasmi Yanga, Saido tayari alisimamishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa kosa la utovu wa nidhami akidaiwa kurudi kambini asubuhi wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya mechi yake muhimu na yenye hamasa ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam dhidi ya mahasimu wao Simba.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi iliyopita Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Feisal Salum au Fei Toto na hivyo kujikatia tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo na sasa inasubiri kuumana na Coastal Union.
Saido mwenyewe aliwahi kunukuliwa kupitia mitandao ya kijamii akipinga kuhusishwa na utovu wa nidhamu akidai kwamba anachafuliwa jina lake na atatoa tamko baada ya mechi dhidi ya Simba, hadi sasa hajafanya hivyo hali inyozidi kuacha maswali kuhusu nini hasa kimemuondoa katika timu hiyo.
Je ni kweli kwamba kiwango cha mchezaji huyo kiko chini? Mchezaji ambaye katika msimu wa Ligi Kuu ya NBC inayokaribia kufikia tamati huku Yanga ikisubiri siku chache zijazo itangaze ubingwa, ameifungia Yanga mabao saba na kutoa asisti nne.
Na vipi kuhusu nidhamu, mbele ya wengi kosa analohusishwa nalo Saido ni kutoweka kambini wakati timu ikijiandaa na mechi dhidi ya Simba, katika hali ya kawaida ukubwa wa kosa hilo unazidishwa na ukweli kwamba ilikuwa mechi dhidi ya Simba, pengine ingekuwa mechi na timu nyingine hali tatizo lisingekuwa kubwa namna hii.
Na je ni kweli kwamba kosa lake ni hilo hilo moja au amekuwa kero katika masuala ya nidhamu lakini uongozi ulimvumilia na mwisho ukapata pa kuanzia yaani kwenye mechi dhidi ya Simba na hapo hapo mkataba ulikuwa ukielekea ukingoni ikawa rahisi kwao kuagana naye.
Katika hilo hilo la mkataba vipi habari zinazoihusisha Simba kumtaka mchezaji huyo, je hizo zimewakera Yanga na hivyo kuona haina sababu ya kukaa na mchezaji ambaye mahasimu wao wanakamilisha mipango ya kumsajili? Hili halina shaka muda utajibu kama anarudi kwao Burundi au anahama kutoka mitaa ya Jangwani na kuelekea mitaa ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.