London, England
Hatimaye hadithi ya kiungo aliyesajiliwa kwa Pauni 89 milioni, Paul Pogba imefikia tamati katika klabu ya Man United baada ya klabu hiyo kuthibitisha kwamba anaondoka mwishoni mwa mwezi huu.
Pogba aliyejunga na Man United mwaka 2016, anaondoka akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kufikia mwisho mwishoni mwa msimu huu huku msimu wake wa mwisho akiandamwa na balaa la kuwa majeruhi ambapo amecheza mechi 27 tu.
Katika taarifa yake Man United imeutaja mwisho wa mchezaji huyo kuwa haukuwa na makuu lakini pia atakumbukwa kwa kuifungia timu hiyo mabao mazuri, asisti za maana na soka la kiwango kizuri.
“Kwa kijana ambaye alijiunga na akademi akiwa na miaka 16 hadi kuichezea United mara zaidi ya 200 huku akibeba taji la vijana, pamoja na mengine mawili ni jambo la kupongezwa na kufurahia,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mara ya kwanza Pogba alijiunga na Man United mwaka 2009 akitokea Le Harve ya Ufaransa wakati huo akiwa na miaka 16 na alikuwa sehemu ya kikosi cha akademi ya Man United kilichobeba taji la vijana mwaka 2011.
Baada ya kucheza mechi saba katika timu ya wakubwa mwaka 2012, mkataba wake ulifikia ukomo na kutimkia katika klabu ya Juventus ya Italia kabla ya kurudi tena Man United mwaka 2016 na sasa anaondoka ingawa haijawekwa wazi anapoelekea.
Katika msimu huu mambo yake hayakuwa mazuri hasa katika mechi dhidi ya Norwich mwezi Aprili ambapo alijikuta akizomewa na baadhi ya mashabiki na baadaye akatolewa.
Akizungumzia kuondoka kwake Man United, Pogba alisema, “Najisikia ufahari kwa kuichezea klabu hii, kuna matukio na kumbukumbu nyingi nzuri lakini kubwa zaidi ni kuungwa mkono na mashabiki bila kuchoka, asante Man United.”
Kimataifa Hatimaye Pogba aondoka Man Utd
Hatimaye Pogba aondoka Man Utd
Related posts
Read also