Barcelona, Hispania
Matarajio ya Man United kumsajili kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong yamegonga mwamba baada ya mchezaji huyo kudai kuwa anapenda kubaki Barcelona.
Awali ilidaiwa kwamba kocha mpya wa Man United, Erik ten Hag alikuwa na shauku kubwa ya kumsajili nyota huyo katika timu yake hasa baada ya kuwa naye pamoja katika klabu ya Ajax ya Uholanzi.
Akizungumzia uamuzi wake, De Jong alinukuliwa akisema, “Napenda kubaki Barcelona, ni timu ya ndoto yangu tangu nikiwa mdogo, sijawahi kuujutia uamuzi wangu licha ya ukweli kwamba nina matarajio makubwa zaidi kuhusu ushindi kuliko ambacho nimepata hadi wakati huu lakini sijawahi kujutia uamuzi wangu.”
Akiwa na Ajax, De Jong alifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu Uholanzi pamoja na kufikia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kunyakuliwa na Barcelona mwaka 2019. Wakati wote huo alikuwa chini ya kocha Ten Hag ambaye kwa sasa anainoa Man United.
Ilitarajiwa kwamba mchezaji huyo angekuwa tayari kwenda Man United kuungana na Ten Hag hasa kwa kuwa mambo katika Barcelona tangu ajiunge na timu hiyo hayajawa mazuri na msimu huu timu hiyo ilimaliza ikiwa ya pili katika La Liga ikiachwa mbali na vinara Real Madrid kwa tofauti ya pointi 13.
Matumaini ya Man United kumpata mchezaji huyo yalikuwa juu hasa kwa kuwa Barcelona inadaiwa kuwa na mpango wa kuuza baadhi ya wachezaji ili kupunguza matatizo ya kifedha yanayowakabili lakini kinachoonekana sasa ni kama vile mchezaji huyo amehakikishiwa mambo yake kuwa mazuri katika kikosi cha timu hiyo.
Kimataifa De Jong aikataa Man United
De Jong aikataa Man United
Related posts
Read also