London, England
Mashabiki wa Liverpool wanaisubiri kwa shauku kubwa mechi yao ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid Jumamosi hii, baada ya mechi hiyo pia watajua hatma ya mshambuliaji wao, Sadio Mane.
Mane ambaye imewahi kuelezwa kuwa na nia ya kuihama Liverpool ili kutafuta changamoto nyingine, ametoa kauli hiyo jana, kauli ambayo bila shaka itawaweka mashabiki wa timu hiyo katika hali ya kusubiri nini kitatokea baaa ya matokeo ya mechi yao na Madrid mjini Paris.
Mshambuliaji huyo kutoka Senegal ambaye alijiunga na Liverpool mwaka 2016 amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho akiwa amefunga mabao 120 hadi sasa na ametokea kuwa mmoja wa wachezaji kipenzi wa mashabiki wa Liverpool.
“Hii hoja ya mambo yangu ya baadaye nitajibu baada ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba fikra zangu ziko kwenye Ligi ya Mabingwa na kushinda taji hilo kitu ambacho ni muhimu zaidi kwangu na kwa mashabiki wa Liverpool,” alisema Mane ambaye amebakiwa na mwaka mmoja katika mkataba wake.
Mane aliongeza kwamba hilo ndilo jibu pekee analoweza kulitoa kwa sasa, “lakini njooni Jumamosi baada ya mechi ya fainali nitawapa jibu zuri mtakalopenda kulisikia, nitawapa jibu ambalo wote mtataka kulisikia.”
Mchezaji huyo pia aliizungumzia mechi yao ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2018 dhidi ya Real Madrid na kusema kwamba Real Madrid ile ilikuwa timu bora lakini akasema kwamba safari hii itakuwa mechi tofauti.
Katika mechi hiyo, Real Madrid iliifunga Liverpool mabao 3-1, mabao yaliyofungwa na Karim Benzema na Gareth Bale aliyefunga mawili wakati bao pekee la Liverpool lilifungwa na Mane.
Kimataifa Hatma ya Mane baada ya fainali
Hatma ya Mane baada ya fainali
Related posts
Read also