Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 jana dhidi ya Mbeya City, sasa wamegeukia maandalizi makali ya mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Azam.
Coastal inatarajia kukipiga na Azam kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Jumapili hii kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Akizungumzia jinsi walivyowazidi ujanja Mbeya City kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Mgunda alisema waliwasoma namna wanavyocheza wakiwa kwao na ameshukuru wachezaji wake wamefuata walichokubaliana na kuibuka na ushindi.
Upande wa maandalizi yake ya Azam, kocha huyo mchezaji wa zamani wa Coastal alieleza kuufahamu vizuri ubora wa Azam na uzito wa mechi za mtoano kama hiyo hasa ukizingatia wanacheza na timu nzuri hivyo wanajua nini cha kufanya ili watinge fainali.
“Hii mechi ya Azam ni tofauti kidogo kwa sababu ni ya mtoano tofauti na ligi kwa hiyo akili zetu zote sasa zimetoka kwenye ligi zinakwenda kwenye mtoano dhidi ya Azam, tunawaheshimu Azam na tunajua itakuwa mechi ngumu na ya ushindani.
“Hii ndiyo mechi ya mwisho kabla ya fainali hivyo tunajua umuhimu wake tunajiandaa kupambana dhidi ya timu bora, lengo letu kuhakikisha tunafanya vizuri hata kwenye mechi hii pia maana ndiyo mechi yenyewe ya kuingia fainali,” alisema Mgunda.
Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itapigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ikizikutanisha Yanga na Simba.
Soka Mgunda aigeukia Azam
Mgunda aigeukia Azam
Related posts
Read also