Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain ya Ligi 1 Ufaransa, Kylian Mbappe anakaribia kutangaza wapi atakwenda msimu ujao wakati huu kukiwa na habari kwamba Real Madrid inahaha kuinasa saini yake.
Mbappe mwenye umri wa miaka 23, mkataba wake na PSG unafikia ukomo majira ya kiangazi msimu huu amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama timu hiyo na kumekuwa na habari za kutatanisha kuhusu kuondoka au kubaki PSG licha ya klabu hiyo kuamini kwamba itambakisha.
Wakati yote hayo yakiendelea, kocha wa PSG, Mauricio Pochettino alinukuliwa mwezi uliopita akisema kwamba ana uhakika wa asilimia 100 kwamba Mbappe atasaini mkataba mpya na klabu hiyo inayomilikiwa na matajiri wa kiarabu.
Habari za ndani zinadai kuwa mazungumzo yanaenda vizuri huko Doha kati ya Rais wa PSG, Nasser al Khelaifi na wawakilishi wa Mbappe na klabu hiyo inaamini inaweza kumshawishi mchezaji huyo akabaki licha ya ukweli kwamba Madrid nao wako kasi katika mbio za kumtaka.
Mara baada ya kutangazwa mwanasoka bora wa mwaka wa Ligi 1 ikiwa ni mara yake ya tatu mfululizo, Mbappe alisema, “Itajulikana hivi karibuni, kila kitu ni kama kimekamilika, ndio uamuzi wangu umeshafikiwa, mambo yako katika hatua za mwisho, ni kwa nini nimekuwa mkimya kidogo, nataka kuheshimu pande zote.”
Habari nyingine zinadai kwamba suala la maslahi ya mchezaji huyo limeendelea kuwa mjadala ndani ya PSG huku Real Madrid, vigogo wa klabu hiyo wakifuatilia kwa karibu mazungumzo hayo kabla ya kuamua pa kuanzia ili kumpata mchezaji huyo.
Soka Mbappe asubiriwa PSG, Madrid yamkomalia
Mbappe asubiriwa PSG, Madrid yamkomalia
Related posts
Read also