na mwandishi wetu
Dar Derby au Kariakoo Derby, mechi ya mahasimu wa soka, Simba na Yanga kwa sasa ni mechi kubwa si Tanzania tu bali hata nje ya mipaka ya Tanzania.
Ni mechi inayotajwa na kujadiliwa nchini Kenya, hasa katika mji wa Mombasa na vitongoji vyake, ni hivyo hivyo Uganda na hapana shaka kwa sasa hali ni hivyo hivyo huko DR Congo.
Kote huko mechi hiyo imekuwa mjadala kwa sababu ya uwapo wa wachezaji mahiri kutoka nchi hizo ambao wamekuwa tegemeo katika vikosi vya Simba na Yanga.
Mfano nani atakataa nafasi ya Joash Onyango katika soka la Kenya, mchezaji huyo anapokuwa akicheza Tanzania, mashabiki wake wa Kenya watapenda kujua nini anafanya na maendeleo yake kwa ujumla na hapo moja ya mechi muhimu kwao ni ile ya mahasimu Simba na Yanga.
Onyango si wa kwanza wamekuwapo kina Ben Mwalala, Boniface Ambani na wengineo ambao ubora wao ulianzia huko walikotoka kabla ya kuuonyesha wakiwa Simba au Yanga na hasa kwenye Dar Derby.
Kwa Uganda nako wapo wengi, mmoja ambaye amekuwa juu zaidi ni Emmanuel Okwi ambaye aliwahi kuichezea Simba pamoja na Yanga lakini anakumbukwa zaidi siku alipoitunga Yanga kwa bao safi la shuti la mbali, bao ambalo lilikuwa kivutio kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa DR Congo nao si haba, mastaa kutoka huko wamejaa Simba na Yanga kiasi kwamba kwa sasa wanaipamba Dar Derby kwa namna ambavyo wamekuwa wakichuana wao kwa wao.
Kwenye Dar Derby ya Jumamosi, mpambano wenye mvuto uliokuwa mjadala kabla na hata baada ya mechi ni ule wa mshambuliaji wa Yanga Mayele na beki wa Simba, Inonga. Mastaa kutoka DR Congo.
Kwa mashabiki wa siku nyingi ukiwatajia mpambano wa Inonga na Mayele unawakumbusha enzi hizo za Athuman Juma Chama, beki kisiki wa Yanga na Zamoyoni Mogela, mshambuliaji mahiri wa Simba.
Enzi hizo ilikuwa ni kawaida kabla ya mechi ya mahasimu, sambamba na matukio mengine, mjadala mmojawapo mkubwa ulikuwa ni namna mafahari hao wawili watakavyochuana, ilikuwa ni Chama na Mogela kabla na hata baada ya mechi kama ambavyo sasa iko hivyo kwa Inonga na Mayele.
Baada ya Chama na Mogela ilikuwa hivyo kwa Hamis Gaga au Gagarino na Athuman China, hii ilikuwa vita inayotajwa kuwa tamu iliyohusisha mastaa wenye vipaji vikubwa ambao walikuwa wakichuana katika dimba la kati, ilikuwa ni mchuano wa ufundi na namna ya kuiongoza timu kupeleka mashambulizi. Ilipopigwa Dar Derby, macho ya ziada ya mashabiki yaliwamulika wachezaji hao kutokana na ufundi wao.
Kwa muda mfupi ikatokea vita nyingine ya winga wa Simba, Damian Kimti na beki wa kushoto wa Yanga, Ken Mkapa, hii haikudumu sana.
Burudani iliyofuata ya mafahari ikiwa kati ya Edibily Lunyamila, winga wa kushoto wa Yanga na Kasongo Athuman beki wa kulia wa Simba, hii nayo ilikuwa gumzo, umahiri wa Kasongo ulipimwa kwa Lunyamila, mchezaji mwingine aliyekuwa na kipaji kikubwa huku akitajwa na baadhi mashabiki kuwa ni mchezaji bora aliyeonyesha uwezo wa hali ya juu wa kuutumia vizuri mguu wa kushoto.
Imekuwa hivyo miaka mingine iliyofuata, wakati wote wamekuwapo mafahari mmoja mmoja ambao ni gumzo katika mechi na wanaozua mjadala miongoni mwa mashabiki.
Baadhi ya mashabiki wa soka wanaweza wakawa wanajiuliza, ni nini hasa kimeifanya vita ya mafahari wawili kuhama kutoka wachezaji wazawa hadi wachezaji wa kigeni, si tena Chama na Mogela bali ni Mayele na Inonga au Mayele na Onyango?
Moja ni ukweli kwamba soka la Bongo linachanja mbuga, linakuwa juu kutokana na uwekezaji hivyo wachezaji mahiri nje ya Tanzania wanataka kucheza soka Tanzania, wanatafuta fursa hizo, ni ajira inayolipa.
Wanapotokea matajiri kuwekeza fedha zao katika soka, nia ni kupata mafanikio kupitia klabu hizo, mafanikio ambayo yataweza kupatikana kukiwa na wachezaji bora.
GSM, anapowekeza fedha Yanga, hafanyi hivyo kama mtu anayetoa sadaka bali anataka mafanikio katika klabu na kwenye biashara zake, mafanikio ambayo yanapatikana kwa kuwa na wacheazaji wazuri. Ni hivyo hivyo kwa Bakhresa, Mo Dewji na wengineo, wanataka kuona matunda ya uwekezaji wao na ndio maana wako tayari kununua wachezaji kwa bei mbaya.
Hata mdhamini mkuu wa ligi hiyo, Benki ya NBC wanafanya hivyo wakipenda kuona thamani ya fedha zao inapaishwa na ubora wa soka kwa timu kusajili wachezaji wazuri.
Tayari kwenye Ligi Kuu ya NBC Bara kuna wachezaji kutoka nje ya Afrika Mashariki, wapo hadi kutoka Afrika Magharibi wameshakuja hadi kutoka Brazil na hapana shaka wataendelea kuja, yote ni katika kutafuta mafanikio.
Wako ambao wanaiona hali hii kuwa inaua vipaji vya wazawa, ni kweli lakini ni jambo ambalo halikwepeki, tupo katika dunia ya ushindani ni lazima wachezaji wazawa watambue hilo kwamba na wao wanatakiwa kupambana kuonyesha uwezo wao na kuwashawishi makocha.
Tunaposema soka biashara au ajira hiyo ndiyo maana yake, ni lazima ishindaniwe, lazima uwepo ushindani kwa lengo la kusaka kilicho bora ambacho kitasaidia kwenye mbio za kusaka mafanikio.
Ni hivyo hivyo katika maeneo mengine, mfano tajiri anapokuwa na kiwanda akiambiwa wafanyakazi wazuri wa kumpa faida wako Zambia au Malawi hawezi kusema hapana nawataka Watanzania tu, atakachofanya ni kuwafata huko huko ili wampe faida.
Kwa hiyo wanaowafikiria wachezaji wazawa, wawakumbushe tu kwamba tupo katika dunia ya ushindani, ni lazima wapambane ili kujiweka katika ubora vinginevyo hakuna timu itakayokataa wachezaji wazuri kutoka nje wakati ina uwezo wa kuwasajili hasa inapotokea mpinzani wake anafanya hivyo.
Soka Kutoka Chama, Mogela hadi Mayele, Inonga
Kutoka Chama, Mogela hadi Mayele, Inonga
Read also
