Na mwandishi wetu
Hawakukosea waliompa Shomary Kapombe jina la utani la ‘Show me the way’ yaani nionyeshe njia. Jana usiku wa Jumapili, Kapombe ni kama vile amewaonyesha Simba njia ya kuelekea nusu fainali.
Ilikuwa ni katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ilikuwa ikiumana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini na kutoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo lilipatikana kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 68 baada ya Benard Morrison kuchezewa rafu akiwa katika eneo la hatari na ndipo Kapombe kwa umahiri mkubwa akaujaza mpira wavuni.
Ushindi wa jana ni hatua ya kwanza nzuri kwa Simba katika safari ya kuelekea hatua ya nusu fainali ambayo Kapombe ni kama vile ameanza kuwaonyesha wenzake njia ya kuelekea huko kwa bao lake mahiri ambalo pia limedhihirisha ile kauli ya mashabiki wa Simba kwamba kwa Mkapa hatoki mtu.
Simba sasa inasubiri kurudiana na Pirates katika mechi ya marudiano ambayo Simba itakuwa ugenini katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini na kama itapata ushindi katika nusu fainali itaumana na mshindi wa mechi kati ya Al Itihhad na Al Ahly Tripoli.

Kwa siku ya leo, mjadala wa mashabiki vijiweni kuhusu mechi hiyo haukwepeki na katika mjadala huo, Kapombe hakwepeki, anaendelea kuwa mjadala kwa mashabiki hao ambao wana kila sababu ya kumjadili hasa kwa kuwa alichokifanya kadhihirisha umahiri na ukomavu wake katika mechi za hadhi ya kimataifa akiwa beki tegemeo wa kulia, amekuwa akifanya hivyo Simba na timu ya Taifa.
Baada ya mwamuzi kuipa Simba penalti, wachezaji wa Pirates walianza kumzonga wakipinga uamuzi huo lakini kwa mashabiki mjadala mdogo na wa muda mfupi wa moyoni na hadharani ulikuwa kuhusu nani angepiga penalti. Kapombe akamaliza hilo kwa kuelekea eneo la kupigia penalti.
Katika kupiga penalti, Kapombe akaonyesha ni kwa nini alijiamini katika hilo, haukuwa upigaji wa kawaida bali upigaji uliojaa ufundi, alimpoteza kipa wa Pirates, Richard Oforji ambaye licha ya kuonekana mwenye kujiamini alijikuta akifuata upepo upande wa kulia huku mpira ukijaa wavuni kupitia upande wake wa kushoto.
Ushindi wa jana haukudhihirisha tu ubora wa Kapombe bali ubora wa Simba kwa ujumla hasa dhamira yao ya kufika mbali katika michuano hiyo na ingawa tayari wameonyesha njia ya kuelekea hatua ya nusu fainali kupitia bao la Kapombe, bado wana mechi ya marudiano itakayoamua hatma yao.
